Magufuli ampa mtihani mgumu aliyemteua kuwa naibu waziri
Ni Naibu Waziri mpya wa Madini Prof Shukrani Manya aliyeteuliwa leo, amtaka kutumia taaluma yake kuikuza sekta ya madini.
- Ni Naibu Waziri mpya wa Madini Prof Shukrani Manya aliyeteuliwa leo.
- Amtaka kutumia taaluma yake kuikuza sekta ya madini.
- Kabla ya uteuzi huo, Prof Munya alikuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Tanzania.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka watendaji wa Wizara ya Madini akiwemo Naibu Waziri mpya wa wizara hiyo, Prof Shukrani Manya kuhakikisha wanatumia utaalam wao kuongeza wigo wa uchimbaji madini Tanzania ili kulinufaisha Taifa.
Prof Manya aliteuliwa leo asubuhi na Dk Magufuli kuwa Naibu Waziri wa Madini na Mbunge. Uteuzi wake umefuatia mteule wa awali, Mbunge wa jimbo la Kilwa Kaskazini, Francis Ndulane kushindwa kuapa.
Kabla ya uteuzi huo, Prof Munya alikuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Tanzania.
Rais Magufuli aliyekua akizungumza leo Desemba 11, 2020 wakati wa uapisho wa naibu waziri huyo jijini Dodoma amesema sekta ya madini ina umuhimu mkubwa, wataalam wa wizara hiyo wakijipanga na kushirikiana wataweza kuikuza zaidi.
“Mkiamua mnaweza kutoa mchango mzuri kwenye Taifa hili,” amesema Rais huku akiwataka wataalam hao kutafakari namna watakavyoipaisha sekta ya madini kwa ujuzi wao.
Ameiagiza wizara hiyo pamoja na Prof Manya kuanza kuangalia uwezekano wa kuchimba madini ya chuma nchini ili kuviwezesha viwanda vya nondo kupata malighafi ya kutosha.
“Tuna chuma, kwanini? hii chuma haiendi kuyeyushwa ikatengeneza nondo badala yake nondo zinatengenezwa kwa mataruma yanayoibwa ya reli. Haya ndiyo maswali magumu mnayotakiwa kuyafanya,” amesema Rais.
Amesema kuna uwezekano madini ya chuma yanaweza kuchimbwa na kuyeyushwa hapa nchini hata kama hayatakua na viwango vinavyotakiwa.
Amebainisha kuwa hiyo itasaidia kuongeza ajira kwa wachimbaji na viwandani.
“Lakini transport sector (sekta ya usafiri) ya kubeba hayo ni pesa, madereva wataajiriwa lakini mwenye kiwanda atatengeneza ajira, Serikali itakusanya revenue (Mapato). Sasa mimi nawaomba kasimamieni pia hili,” amesisitiza mkuu huyo wa nchi.
Zinazohusiana:
- Rais Magufuli asema Uchaguzi Mkuu hautaihirishwa
- Maagizo makuu 3 ya Rais Magufuli kwa watendaji serikalini
- Rais Magufuli ateua Mwenyekiti mpya Bodi ya uwekezaji wa mapato ya mafuta na gesi
Pia ameagiza wataalam hao kuangalia namna makaa ya mawe yanavyoweza kutumika kutengeneza umeme utakaotumiwa kwenye viwanda vikiwemo vya saruji ambavyo siku za hivi karibuni vilikua vinakabiliwa na changamoto ya uzalishaji.
“Sasa ni jukumu la ninyi Wizara ya Madini kujipanga vizuri mkafanye kazi usiku na mchana ili ukombozi na zawadi tuliyopewa na Mwenyezi Mungu ya kupewa madini mengi ya kutosha yaanze kutumika,” amesema.
Aeleza sababu za kumchagua Prof Manya
Rais ameeleza kuwa Prof Manya amechaguliwa kuwa Naibu Waziri ili kuwa kiungo na kuongeza nguvu katika wizara hiyo ambayo inaongozwa na Waziri Doto Biteko ambaye kitaaluma ni mwalimu.
“Tumekuchagua wewe kwenda kuwa Naibu Waziri kwa wizara hii tuliona kwenye nafasi za juu inayumba kwa sababu waziri hajui madini, yeye taaluma yake ni mwalimu,” amesema Rais.
Amemtaka kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana na watendaji wa madini kwa kutumia uwezo wao kuipeleka mbele sekta ya madini.