October 6, 2024

Magufuli amuongezea DPP siku saba kupokea barua za watuhumiwa uhujumu uchumi

Rais John Magufuli ameongeza siku saba kwa watuhumiwa wa uhujumu uchumi ili kufikisha maombi ya kukiri makosa na kulipa fedha za umma katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP).

  • Ni za wale ambao wako tayari kukiri makosa yao na bado hazijamfikia ofisi. 
  • Mpaka sasa watuhumiwa 467 wameandika barua.
  • Sh107.8 bilioni zitalipwa na watuhumiwa watakaosamehewa.
  • Rais Magufuli awananga Mawakili wanaozauia watuhumiwa wasiombe msamaha.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameongeza siku saba kwa watuhumiwa wa uhujumu uchumi ili kufikisha maombi ya kukiri makosa na kulipa fedha za umma katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP).

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Septemba 30, 2019), Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akipokea ripoti ya utekelezaji wa ushauri alioutoa Septemba 22, 2019 wa kuwaachia huru watuhumiwa wa uhujumu wa uchumi walio tayari kuandika barua za kukiri makosa yao na kulipa fedha wanazotuhumiwa. 

Hatua ya Dk Magufuli ya kuongeza muda, imekuja baada ya DPP, Biswalo Mganga kueleza kuwa baadhi ya barua hazikumfikia katika ofisi yake kutokana na kukwama katika ofisi za mikoa na magereza nchini Tanzania.

DPP Mganga amemuomba Rais amuongezee siku tatu ili ashughulikie barua ambazo bado hazijamfikia. 

Wakati Rais Magufuli akijibu ombi hilo, amesema ameongeza siku saba badala ya tatu kuanzia leo Septemba 30 hadi Oktoba 6, 2019 kwa watuhumiwa kuwasilisha barua zao na ofisi ya DPP kukamilisha zoezi hilo la uchambuzi wa barua. 

“Mimi naona nikupe siku saba ili usije ukaniomba tena siku zingine. Nilitoa siku hizo sita siku za nyuma kwamba watuhumiwa wote wanaotaka kupata huu msamaha kwa kupitia process (mchakato) za kisheria na wameitikia watu zaidi ya 467 na fedha Sh107.842 bilioni zitaokolewa na nina uhakika hawatarudia makosa yao mimi nafikiri niwaongezee siku saba zaidi,” amesema Magufuli.

“Hizi siku saba zinazokuwa extended (zinazoongezwa) ni kwa wale ambao wamekwama barua zao wameandika ziko magerezani hazijakufikia,” amesisitiza Rais Magufuli. Picha| Ikulu

Aidha, ametoa angalizo kwa wale wote ambao watashikwa na makosa ya uhujumu uchumi baada ya zoezi hilo, kuwa watachukuliwa hatua za kisheria kwani kupitia msamaha huo siyo kwamba amefuta kesi za uhujumu uchumi.

“Baada ya siku hizi ambazo tumeziweka, wale wote watakaoshikwa kwenye masuala ya uhujumu uchumi, sheria ichukue mkondo wake. Isije sasa ikawa imejengeka mazoea kwamba kesi ya uhujumu uchumi haipo.

“Hizi siku saba zinazokuwa extended (zinazoongezwa) ni kwa wale ambao wamekwama barua zao wameandika ziko magerezani hazijakufikia,” amesisitiza Rais Magufuli.


Zinazohusiana


Katika hatua nyingine, amesema wapo watuhumiwa wanaodanganywa na Mawakili wao kuwa msamaha huo uliotolewa ni wa uongo. 

Amesema wasidanganyike kwani huenda ikawa ni mbinu ya Mawakili hao kutaka kuendelea “kuwachomoa pesa” na baada ya msamaha huo hapatakuwepo na msamaha mwingine.

“Huwezi ukatoa msamaha wa majaribio. Huwezi ukatoa msamaha wa kumtega mtu. Msamaha ukishautoa ni msamaha,” amesema Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa DPP Mganga, watuhumiwa walioomba msamaha na kukubali kurudisha fedha hizo ambazo ni zaidi ya Sh107 bilioni ni 467 mpaka sasa.

Kati ya fedha hizo, Sh13.6 bilioni zitalipwa papo kwa papo huku kiasi kilichobaki cha Sh94.2 bilioni, watuhumiwa wamesema watalipa kwa awamu.

Ofisi ya DPP imetakiwa kushirikiana na mamlaka zingine zikiwemo Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi na Magereza ili washtakiwa hao waanze kutoka  ili wakajumuike na familia zao.