July 3, 2024

Magufuli ataka kesi za mikopo ya benki kumalizwa haraka Tanzania

Amesema itasaidia kupunguza athari za kiuchumi kwa Taifa ikiwemo kupungua kwa uwezo wa benki kutoa mikopo kwa Watanzania.

  • Ni zile zinazofunguliwa na wateja wa benki wanaodaiwa mikopo.
  • Amesema hali hiyo inapunguza kasi ya utoaji wa mikopo na shughuli za maendeleo. 
  • Aitaka Mahakama kuharakisha usikilizwaji wa kesi hizo. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameitaka Mahakama ya Tanzania kuharakisha usikilizwaji wa kesi za wadaiwa wa mikopo ya benki ili kupunguza athari za kiuchumi kwa Taifa ikiwemo kupungua kwa uwezo wa benki kutoa mikopo kwa Watanzania. 

Rais Magufuli ameeleza leo Februari 1, 2021 kwenye kilele cha Wiki ya Sheria jijini Dodoma kuwa ipo tabia ya baadhi ya wateja wa benki kukimbilia mahakamani kufungua kesi nyingi au kuweka mazuio kwa lengo la kuchelewesha kulipa mikopo wanayodaiwa na benki.

“Changamoto nyingine ni kuhusu ucheleweshaji wa kesi, hivi punde nimetoka kuipongeza Mahakama kupunguza ucheleweshaji wa kesi, hata hivyo, tatizo bado lipo hususan kwenye mashauri yanayohusu masuala biashara na mikopo,” amesema Dk Magufuli.  

Kesi za namna hiyo, amesema, ziko nyingi na nyingine zina miaka mitano hazijaamriwa, jambo ambalo linazuia Watanzania wengine kupata mikopo.

“Hapa naomba nitoe mfano wa kesi zilizofunguliwa mahakamani na wateja wakubwa wa benki ndogo tatu: TPB, Azania Bank Limited na Benki ya Maendeleo ya TIB. Kwa mujibu wa taarifa za 31 Desemba, 2020, Azania Bank ina kesi 36 zilizofunguliwa na wadaiwa wake zenye thamani Sh352.27 bilioni.

“Benki ya Maendeleo (TIB) ina kesi 44 zenye thamani ya Sh167.267 bilioni na TPB ina kesi 16 zilizofunguliwa na wadaiwa wake zenye thamani ya Sh6.2 bilioni. Hivyo kufanya mashauri yaliyofunguliwa na wadaiwa wa benki hizo kufikia bilion 525.74,” amesema Rais Magufuli.  

Ameitaja benki nyingine kuwa ni CRDB ambayo ina kesi 282 zenye thamani ya Sh400 bilioni. 


Zinazohusiana: 


Athari za kesi hizo

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema hali hiyo ya wadaiwa kukimbilia mahakamani na kesi kuchelewa kutolewa maamuzi imekua na athari nyingi kuichumi kwa Tanzania ikiwemo kupungua kwa uwezo wa benki kutoa mikopo kwa wateja, kuongezeka kwa gharama za riba kutokana na benki kuongeza riba kufidia mikopo chechefu.

“Lakini tatu ni kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kutokana na benki kulipa riba kwa amana zilizotumika kutoa mkopo kwa mteja wenye madeni ambao wamekimbilia mahakamani na kesi zao kutotolewa maamuzi mapema,” amesema Rais. 

Amesema athari nyingine ni kiasi kikubwa cha fedha kuendelea kushikiliwa na wadaiwa sugu ambao wamefungua kesi mahakamani badala ya fedha hizo kutumika kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo ingechochea ukuaji wa uchumi.

“Napenda kutoa wito kwa mahakama kuliangalia suala hili vizuri, kesi za namna hii ingefaa zishughulikiwe mapema ili zisiathiri ukuaji wa uchumi wa nchi yetu,” amesema Dk Magufuli. 

Amesema uchumi utajengwa kama kutukua na taasisi imara za kifedha ikiwemo benki zenye ukwasi wa kutosha kwa ajili ya kutoa mikopo ya muda mrefu yenye riba nafuu kwa wananchi.  

Mahakama ni moja ya chombo huru ambacho umpa fursa mkopaji au taasisi ya kifedha fursa ya kutatua migogoro inayoibuka kati yao iwapo watashindwa kumalizana wenyewe katika masuala yanayohusu mkopo.