July 5, 2024

Magufuli atoa maagizo mazito usafirishaji magogo nje ya Tanzania

Aitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuachana na utaratibu wa sasa wa kuuza magogo nje ya nchi na badala yake vianzishwe viwanda vya ndani vya bidhaa hiyo.

  • Aitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuachana na utaratibu wa sasa wa kuuza magogo nje ya nchi.
  • Aagiza vianzishwe viwanda vya bidhaa za miti ili kutengeneza fursa za ajira na kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.
  • Awataka Watanzania kuepuka ukataji wa miti. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia uwezekano wa kuachana na utaratibu wa sasa wa kuuza magogo nje ya nchi, badala yake vianzishwe viwanda vya ndani vya  bidhaa za miti ili kutengeneza fursa za ajira na kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa. 

 Amesema kusafirisha magogo nje ya nchi kunaifanya nchi ikose mapato na ajira za Watanzania zinaenda kwa watu wengine na kuikosesha nchi maendeleo yaliyokusudiwa. 

“Ni lazima tuachane na utaratibu wa sasa wa kuuza nje magogo, bahati nzuri kule kwenye magogo nako tunalalaliwa sana na hili pamoja Kamishna (Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS), Prof.Dos Santos Silayo) na kukupongeza kupanda miti, hili suala la kusafirisha magogo uweke nguvu za kutosha,” amesema Dk Magufuli

Rais ametoa maagizo hayo wakati akizindua shamba la miti la Silayo lenye ukubwa wa hekta 69,000 lilipo wilayani Chato mkoani Geita  leo Januari 27. 

Shamba hilo lililoanzishwa miaka minne iliyopita ni la pili kwa ukubwa nchini na limeajiri Watanzania 800 katika shughuli mbalimbali. 

“Ni vyema basi tujipange katika siku za usoni kuhakikisha hizi mali ikiwemo misitu yetu inatumika hapa hapa kwa kutengeneza vifaa vinavyotokana na misitu ili nchi iweze kupata fedha nyingi zaidi,” amesema.


Soma zaidi:


Atoa maagizo mazito kwa watendaji serikalini

Ameigiza Wizara ya Maliasili na Utalii, TFS pamoja na wadau wengine ikiwemo Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) kuhakikisha inawajengea uwezo vijana kujihusisha na shughuli za kutengeneza bidhaa za miti wakiwemo mafundi selemala.

“Hakikisheni mnawapatia ujuzi na mitaji ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ubora zaidi. 

“Mkiwawezesha vijana wetu hatutakuwa tunaagiza samani kutoka nje kama ilivyo sasa na badala yake samani zote zitatengenezwa hapa na hatatumia fedha za kigeni kuagiza bidhaa hizo,” amesema Rais Magufuli.  

Pia ameagiza kuwatengenezea mazingira mazuri ya biashara wafanyabiashara wadogo wanaojihusisha na biashara ya miti  kwa Halmashauri kuacha kutoza kodi kubwa na kuwabughuza wakati wakifanya shughuli zao. 

Kwa wananchi, Rais amewataka kuachana na tabia ya kukata na kuchoma miti hovyo, kuvamia maeneo ya hifadhi huku akihimiza taasisi za umma na binafsi kupanda miti katika maeneo yao kujiongezea kipato na kutunza mazingira.