Magufuli atoa tena maagizo mazito mradi wa nyumba za NSSF Kigamboni
Magufuli ametoa maagizo hayo leo (Februari 11, 2020) wakati akizindua majengo ya Manispaa na ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam huku akisisitiza umuhimu wa wafanyakazi hao kuishi karibu na wananchi wanaowahudumia.
- Aagiza watumishi serikalini wahamie kwenye nyumba hizo ndani ya wiki moja.
- Watakaa humo bure kwa kipindi cha mwaka mmoja.
- Asema itawarahisishia wananchi wa Kigamboni kuwapata watumishi hao pale wanapowahitaji.
Dar es Salaam. Rais Magufuli ameagiza watumishi wa Halmashauri ya Kigamboni wahamie kwenye majengo ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) yaliyopo wilayani Kigamboni ndani ya wiki moja, lengo likiwa ni kuwasogeza karibu na wananchi wa wilaya hiyo.
Mradi wa nyumba hizo 7,460 upo katika eneo la Dege Beach ni katika Wilaya hiyo.
Magufuli ametoa maagizo hayo leo (Februari 11, 2020) wakati akizindua majengo ya Manispaa na ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam huku akisisitiza umuhimu wa wafanyakazi hao kuishi karibu na wananchi wanaowahudumia.
Akielekeza maagizo kwa viongozi wa halmashauri hiyo, Magufuli amesema watumishi hao wataishi kwenye nyumba hizo bure kwa mwaka mzima wakati ujenzi wa nyumba zingine za Serikali ukiendelea.
“Huwezi ukawa unafanya kazi Kigamboni ukawa unakwenda kulala Temeke au Kinondoni. Lazima sasa ndani ya wiki hii muhamie kukaa kigamboni,” amesema Magufuli.
Magufuli amesema majengo hayo ni ya Selikali hivyo ipo haja ya majengo hayo kutumika kwa ajili ya maslahi ya wananchi.
“Hatuwezi tukawa tunakaa na nyumba za NSSF au za Wizara ya Mheshimiwa Mhagama hazina watu wakati wafanyakazi wa wilaya hii mpya hawana mahali pa kukaa,” amesema Rais Magufuli.
Zinazohusiana
- Rais Magufuli amfukuza kazi aliyechana kitabu cha dini Kilosa
- Mawakili wa Serikali waomba kuzungumza na Kabendera
Pamoja na hayo, Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo kutafuta kiasi cha Sh2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Serikali katika eneo mojawapo katika wilaya hiyo.
Ujenzi huo unatarajiwa kuwa wenye manufaa kwa watumishi hao pale mwaka waliopewa utakapoiisha.
Magufuli amesema watumishi hao wakiahamia katika nyumba za NSSF, watasogea karibu na wananchi na itakuwa rahisi kuwahudumia.
Maagizo hayo yanayohusisha majengo ya NSSF ni muendelezo wa maagizo ambayo Rais Magufuli aliyatoa Juni, 2019 baada ya kupendekeza wananchi wa Kigamboni kujadili endapo mradi huo ugeuzwe mabweni au makazi ya wafanyakazi wa umma.
Desemba 29, 2020, NSSF ilisaini makubaliano na vyuo vya elimu ya juu vilivyopo Dar es Salaam vya Chuo Kikuu cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kwa ajili ya kuwapangisha wanafunzi nyumba za shirika hilo zilizopo Mtoni Kijiji.