November 24, 2024

Magufuli atoa ujumbe mzito uzinduzi kitabu cha Mkapa

Rais John Magufuli amewataka viongozi wastaafu katika ngazi mbalimbali kuandika vitabu vinavyoelezea maisha yao ili kuwa chachu kwa Watanzania na viongozi wa sasa wanaoibukia kwenye uongozi.

  • Amesema waandike vitabu vinavyoelezea maisha yao ili kuwa chachu kwa Watanzania na viongozi wa sasa wanaoibukia kwenye uongozi. 
  • Wawataka Watanzania kujenga na kupenda utamaduni wa kujisomea.
  • Aeleza alivyonyweshwa sumu wakati wa uongozi wa Rais Mkapa.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka viongozi wastaafu katika ngazi mbalimbali kuandika vitabu vinavyoelezea maisha yao ili kuwa chachu kwa Watanzania na viongozi wa sasa wanaoibukia kwenye uongozi. 

Dk Magufuli alikuwa akizungumza leo (Novemba 12, 2019) katika uzinduzi wa kitabu cha “My Life, My Purpose” kilichoandikwa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kikielezea maisha yake binafsi na uzoefu wake katika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo nafasi ya urais aliyoshika kati ya mwaka 1995 hadi 2005. 

Rais amesema kitabu hicho ni muhimu sana kwa Watanzania na viongozi wanaoibukia kujifunza misingi ya uongozi na kuepuka makosa waliyofanya viongozi waliotangulia katika kutimiza majukumu ya kuwaletea wananchi maendeleo. 

“Niwahimize wastaafu wengine kuiga mfano wa mzee Mkapa waandike vitabu ili uzoefu wao katika uongozi uwe chachu kwa vijana wetu wanaoibukia kwenye uongozi. Nimefurahi kusikia kuwa mchakato wa kukamilisha kitabu cha maisha ya mzee Mwinyi (Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi) upo mbioni kumamilika na mzee Kikwete naye anaendelea na uandishi wa kitabu chake,” amesema Rais Magufuli.

Amesema uandishi huo wa vitabu usiishie kwa viongozi wastaafu kwa nafasi za urais, “ tunataka na viongozi wengine” wa ngazi mbalimbali za uongozi waliowahi kulitumikia Taifa.

Aidha, ameitaka taasisi ya Uongozi (UONGOZI Institute) kuendeleza mradi wao wa kuweka kumbukumbu za viongozi na Taifa ili kupitia vitabu  Watanzania wafahamu kwa undani historia ya uongozi nchini. 

Ameitaka taasisi hiyo kutafsiri kitabu cha Mkapa kwa lugha ya Kiswahili ili kiweze kuwafikia watu wengi ambao hajui lugha ya Kiingereza. 

“Napenda kuwahimiza Watanzania kujenga na kupenda utamaduni wa kujisomea. Vitabu haviwezi kuwa na manufaa yoyote endapo havitasomwa,” amesema Rais katika uzinduzi huo uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNCC) na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali na taasisi mbalimbali. 


Soma zaidi:


Katika hatua nyingine, Rais amewataka Watanzania wote kuwaenzi na kuwaheshimu viongozi waliostaafu pamoja na wazee wengine wote kwa sababu ni hazina kubwa ya Taifa na wana mengi ya kuwafunza.

“Kwa upande wetu Serikali tunahidi kuendelea kuwaenzi wazee wote nchini wakiwemo viongozi wetu wastaafu. Mwisho napenda kutoa witi kwa Watanzania kuendelea kudumisha umoja na mshikamano wetu kama Taifa. Tuwe na muelekeo mmoja kama Taifa na kamwe tusikubali kuyumbishwa na mtu yoyote,” amesisitiza Rais.

Asimulia alivyochukiwa na viongozi wenzake

Akielezea jinsi alivyofanya kazi na Mkapa, Rais Magufuli amesema amejifunza mengi kutoka kwake ikiwemo kuwa na ujasiri na kufanya kazi kwa bidii hata kama unachukiwa na watu. 

“Nilipofanya kazi vizuri Mzee Mkapa hakusita kunisifia na sitosahau siku aliyotangaza kuwa, Mimi ni askari wake. Baada ya kutangazwa hivyo nilichukiwa na viongozi wengi hadi kufikia hatua ya kunyweshwa sumu Dodoma, `al-manusura’ sumu hiyo iondoe uhai wangu,” amesema na kubainisha kuwa,

”Kwa kiasi kikubwa Mzee Mkapa alinijengea ujasiri na kujiamini pale aliponiteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, kwa mzee Mkapa wateule wake wote ni sawa, hakuna mkubwa wala mdogo.”

Rais John Magufuli (wa pili kushoto) akiwa na marais wastaafu, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Zanzibar, Ali Mohammed Shein katika uzinduzi wa kitabu cha “My Life, My Purpose” jijini Dar es Salaam. Picha|Mtandao.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais mstaafu Mkapa amesema haikuwa rahis kufikia uamuzi wa kuandika kitabu hicho lakini ameandika kitabu hicho kwa sababu kuu tatu ikiwemo unyeti wa nafasi ya urais aliyowahi kuishika na heshima ya kuitumikia nchi kwenye nafasi ya juu kabisa.

“Pili katika historia yangu kuna wengi sana ambao wamechangia kwa namna moja ama nyingine kwenye maisha yangu na uongozi wangu. Nimeona kitabu hiki kitanipa fursa ya kuwashukuru kwa pamoja kwa mchango wao kwa maisha yangu binafsi lakini pia kwenye uongozi wangu wa Taifa letu,” amesema Mkapa.

Mkapa amesema pia ni fursa ya kuelezea kwa mtazamo wake masuala mbalimbali hasa kuhusu ukombozi wa bara la Afrika na changamoto za uongozi wa bara hilo ambazo alizielewa na kuziona wakati anafanya kazi na Mwalimu Julius Nyerere. 

Kuzinduliwa kwa kitabu cha “My Life, My Purpose” kunaenda sambamba na kusheherekea siku ya kuzaliwa kwa Rais mstaafu Mkapa ambaye leo ametimiza miaka 81. 

Alizaliwa Novemba 12, 1938 katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara na amewahi kushika nafasi mbalimbali serikalini kabla ya kuwa Rais mwaka 1995.