November 24, 2024

Magufuli awalilia wafanyakazi wa Azam Media waliofariki kwa ajali

Amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa kampuni za Said Salim Bakhresa kufuatia vifo vya wafanyakazi watano wa vyombo vya habari vya Azam Media Limited.

  • Amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa kampuni za Said Salim Bakhresa kufuatia vifo vya wafanyakazi watano wa vyombo vya habari vya Azam Media Limited.
  • Ajali hiyo imeangamiza maisha ya watu saba wakiwa wafanyakazi watano wa Azam Media.
  • Wafanyakazi hao walikuwa wakielekea katika uzinduzi wa hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa kampuni za Said Salim Bakhresa kufuatia vifo vya wafanyakazi watano wa vyombo vya habari vya Azam Media Limited na kuwataka watumiaji wa barabara kuzingatia sheria ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika. 

Wafanyakazi hao watano ni sehemu ya watu saba wakiwemo dereva na msaidizi wake waliofariki dunia katika ajali hiyo iliyotokea leo (Julai 8, 2019) majira 2:30 asubuhi katika eneo la Kizonzo, katikati ya Igunga mkoani Tabora na Shelui (Singida).

Katika ajali hiyo gari aina ya Toyota Coaster lililowabeba wafanyakazi wa Azam Media Limited kuelekea Mwanza liligongana na lori la mizigo lililokuwa linaelekea Jijini Dar es Salaam. 

Wafanyakazi hao walikuwa wanatoka Dar es Salaam kwenda kwenye sherehe za uzinduzi wa hifadhi mpya ya Taifa ya Burigi-Chato kwa ajili ya kurusha moja kwa moja matangazo ya sherehe hizo.

“Nimeshtushwa na vifo hivi, nampa pole Mwenyekiti Ndg. Said Salim Bakhresa, ndugu wa marehemu wote, Mkurugenzi Mkuu, Ndg. Tido Muhando na wafanyakazi wote wa Azam Media Ltd, waandishi wa habari na wote walioguswa na vifo hivi,” imeeleza taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa. 


Zinazohusiana:


Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais amewaombea marehemu wote wapumzike mahali pema peponi. 

Aidha, Rais amewaombea majeruhi  watatu wa ajali hiyo wapone haraka ili waendelea kutimiza majukumu yao ya kila siku. 

Hata hivyo, Rais Magufuli amerejea wito wake wa kuwataka watumiaji wa barabara hususan madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarabi ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika. 

Watu na taasisi mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali wametoa salamu za pole kwa uongozi wa Azam Media kwa kuondokewa na wafanyakazi hao.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amesema ameshtushwa sana baada ya kusikia taarifa za ajali hiyo na wanafanya kila liwezekanalo kuwasaidia majeruhi wa ajali hiyo. 

“Moyo wangu umeshtuka na unatoa machozi ya damu kupata taarifa za kushtua na kusikitisha za ajali ya wafanyakazi wa @azamtvtz iliyotokea maeneo ya Malendi, Singida na kuchukua maisha ya 7 kati ya 10 waliokuwepo. Tunahangaika kutafuta usafiri wa haraka wa majeruhi hao 3!,” ameandika Dk Kigwangalla katika ukurasa wake wa Twitter.

“Hili ni pigo kubwa kwa wenzetu wa Azam Media na tasnia ya habari kwa ujumla. Tumepoteza nguvukazi muhimu katika kulihabarisha Taifa. 

“Tunawapa pole Azam Media, ndugu na jamaa kwa kuondokewa na wapendwa wao na Mungu awape pumziko la milele marehemu wote na kuwaponya majeruhi wote wa ajali hiyo,” amesema Nuzulack Dausen, Mkurugenzi Mtendaji na Mhariri Mkuu wa Nukta Africa.

Nukta Africa huchapisha habari katika mtandao wa Nukta (www.nukta.co.tz).