November 24, 2024

Magufuli awapa siku tano Kigwangalla na katibu wake kumaliza tofauti zao

Rais wa John Magufuli ametoa siku tano kuanzia leo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda kuondoa tofauti zao vinginevyo atatengua uteuzi wao.

  • Amesema wasipopatana na kuanza kuzungumza atatengua uteuzi wao.
  • Amesema kutokuelewana kwa viongozi hao kumesababisha baadhi ya shughuli za wizara kusuasua.
  • Ameiongezea muda Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) iliyomaliza muda wake.

Dar es Salaam. Rais wa John Magufuli ametoa siku tano kuanzia leo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla na Katibu Mkuu wa wizara hiyo,  Profesa Adolf Mkenda kuondoa tofauti zao vinginevyo atatengua uteuzi wao.

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Desemba 31, 2019) na askari wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita, amezungumzia masuala mbalimbali ikiwamo kwa wateule wake wa wizara hiyo kuelewana lasivyo atatengua uteuzi wao.

Amesema kutokuelewana kwa viongozi hao kumesababisha baadhi ya shughuli za wizara kusuasua, jambo linaloweza kukwamisha ukuaji wa sekta ya utalii kwa wakati.

“Ninafahamu watendaji wenu wa juu, katibu mkuu na waziri kila siku wanagombana na ninawatazama taratibu, nilishampa kazi Katibu Mkuu Kiongozi awaite awaeleze lakini wasipobadilika nitawaondoa,” amesema Rais.

Ameongeza kuwa Katibu Mkuu hataki kumheshimu Waziri na Waziri hataki kwenda pamoja na Katibu Mkuu na hivyo hawezi kuwa na viongozi wasioelewana katika wizara moja.

“Kwahiyo nalizingumza hili leo tarehe 31 ya mwezi wa 12 (2019) kwamba wajirekebishe, ikiwezekana wajirekebishe ndani ya siku tano, wawe wanasalimiana, wanazungumza, mimi nina vyombo ninafahamu nani hafai zaidi,” amesema Rais Magufuli katika taarifa iliyotolewa leo na Karugenzi ya Mawasiliano Ikulu.


Soma zaidi:


Rais Magufuli amekuwa Rais wa kwanza wa Taifa hilo kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita akiwa madarakani.

Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo ipo Kusini Magharibi mwa Ziwa Victoria mkoani Geita. Mwaka 1965 kisiwa hicho kilipewa hadhi ya kuwa Pori la Akiba ambapo zoezi la kupandikiza wanyama lilianza katika maeneo yaliyoko nje ya kisiwa na mwaka 1977 ilipewa hadhi ya kuwa Hifadhi ya Taifa.

Kwa mujibu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Rubondo ina ukubwa wa kilomita za mraba 456 ambapo kilomita za mraba 220 ni eneo lenye maji wakati kilomita 237 ni nchi kavu. 

Upekee wa Hifadhi hiyo ni uwepo wa visiwa vingine 11 ambavyo ni Izilambuba, Kalera, Rubiso, Makozi, Irumo, Mizo, Chambuzi, Chitebe, Manyila, Chitende na Nyamitundu ambavyo vinapambwa na vivutio mbalimbali.

Utajiri mkubwa Hifadhi ya Taifa ya Rubondo ni uwepo wa misitu ya asili ambayo inatoa makazi kwa wanyamapori wa aina mbalimbali wakiwemo Tembo, Twiga, Mbega mweusi na mweupe, Suni na ndege mbalimbali. Pia ni moja ya maeneo muhimu ya mazalia ya ndege wahamao pamoja na jamii ya samaki ya Tilapia

Aidha, Rais Magufuli ameiongezea muda Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) iliyomaliza muda wake chini ya Mwenyekiti Jenerali Mstaafu George Waitara kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Tanapa katika uhifadhi wa maliasili.

Pia ameipongeza kwa kuunda Jeshi la Usu la Askari Wanyamapori katika kupambana na uhalifu unaofanywa katika hifadhi za wanyamapori.