July 3, 2024

Mahindi ya Tanzania sasa yapata soko Misri

Kuanzia Julai 2021 wakulima wataanza kuuza tani milioni 1 za mahindi kwa kampuni ya Smart Group ya Misri.

  • Ni soko la mahindi ya njano yanayotumika kutengeneza chakula cha mifugo.
  • Kuanzia Julai 2021 wakulima wataanza kuuza tani milioni 1 za mahindi kwa kampuni ya Smart Group ya Misri.
  • Serikali kuwahamasisha wakulima kulima kwa wingi zao hilo. 

Dar es Salaam. Wakulima wa mahindi ya njano nchini Tanzania sasa wana kila sababu ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo baada ya kupatikana kwa soko la uhakika nchini Misri.

Mahindi hayo yana virutubisho vingi ikiwemo vitamin A vinavyosaidia kuzuia upofu na kukinga mwili dhidi ya magonjwa ya kisukari, moyo na saratani. Mahindi hayo hutumika pia kutengeneza maarufu ya bisi.

Kuanzia Julai 2021 wakulima wataanza kuuza mahindi hayo kwa kampuni ya Smart Group ya Misri ambayo inahitaji tani milioni 1 za mahindi kutoka Tanzania kila mwaka. 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya amesema mahindi ya njano yanayotakiwa na kampuni hiyo ni kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha chakula cha mifugo na samaki

Kusaya katika taarifa yake iliyotolewa usiku wa Novemba 16, 2020 amesema mahitaji hayo yanatoa fursa ya soko la Tanzania kukua kwa sababu Watanzania wengi hawazalishi wala kula mahindi ya njano. 

“Kwa sasa uzalishaji wa mahindi ya njano ni mdogo  kutokana na Watanzania wengi kutotumia mahindi haya kama chakula.

Kufuatia makubaliano hayo na Smart Group, Kusaya amesema  watahamasisha wakulima kuanzia msimu huu Novemba walime kwa wingi kutokana na kuwepo uhakika wa soko.

Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula ambayo hutegemewa na Watanzania kupata chakula na kujiingizia kipato kwa ajili kuboresha maisha yao. 


Zinahusiana: 


Mwenyekiti wa Kampuni ya Smart Group, Yasser Attia amesema nchi yake inahitaji mahindi ya njano takriban tani milioni nane kwa mwaka ambayo kwa sasa yanaagizwa zaidi kutoka Argentina na Ukraine.

“Tumekuja Tanzania tukiamini ni ndugu zetu tunategemea kuongeza zaidi mahusiano ya kibiashara ili wakulima wa mahindi wazalishe zaidi na kupata faida kupitia ushirikiano huu na Misri,“ amesema Attia.

Mbali na mahindi, Misri inaangalia uwezekano wa kununua mazao mengine ya Tanzania yakiwemo maparachichi, mananasi, papai, viungo, kahawa, korosho na chai.

Hata hivyo, Attia amesema ununuzi wa mazao hayo utategemea ubora na gharama za usafirishaji mazao hayo kutoka Tanzania hadi Misri kwa njia ya bandari.

Hiyo siyo mara ya kwanza kwa Tanzania kuuza mahindi nje ya nchi, imewahi kufanya hivyo kwa nchi za Zimbambwe, Malawi na Congo DRC.  

Katika msimu wa mwaka 2018/2019 uzalishaji wa mahindi ulifikia tani milioni 5. 65 sawa na asilimia 71 ya lengo la tani milioni 8. 

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga katika hotuba ya bajeti ya wizara yake ya mwaka 2020/21 alisema lengo lililowekwa halikufikiwa kutokana na upungufu wa mvua za vuli na mvua za msimu kwa baadhi ya mikoa inayopata mvua hizo.