Majaliwa aagiza kupitiwa upya kwa tozo za watalii
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza wadau wa masuala ya utalii nchini wafanye mapitio ya gharama za huduma wanazowatoza watalii na amesisitiza kuwa si sahihi kuwatoza wazawa kwa kutumia fedha za kigeni au gharama sawa na wageni.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akimshika kobe, wanaohifadhiwa katika hifadhi ya Jozani, mkoani Kusini Unguja. Januari 17, 2020. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Asema si sahihi kuwatoza wazawa kwa fedha za kigeni.
- Asema jambo hilo linazuia wazawa kushiriki kikamilifu katika shughuli za utalii.
- Tanapa yaweka wazi viwango vya tozo vinavyotakiwa kutozwa kwa watalii.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza wadau wa masuala ya utalii nchini wafanye mapitio ya gharama za huduma wanazowatoza watalii na amesisitiza kuwa si sahihi kuwatoza wazawa kwa kutumia fedha za kigeni au gharama sawa na wageni.
Majaliwa amesema kuwa kuna baadhi ya maeneo ya kutolea huduma za kitalii wazawa wanatozwa gharama sawa na wageni, jambo linazuia wazawa kushiriki kikamilifu katika shughuli za utalii.
“Kitendo cha kuwatoza wazawa gharama sawa na wageni kitasababisha baadhi kushindwa kutembelea maeneo hayo,” amesema katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu leo (Januari 18, 2020) katika ziara yake visiwani Zanzibar.
Amewataka wadau wa utalii kwa kushirikiana na Serikali waandae viwango maalumu kwa ajili ya wazawa na kutengeneza mazingira mazuri yatakayohamasisha utalii wa ndani.
Zinazohusiana:
- Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni.
- Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii
- Tanzania yang’ara tena tuzo za eneo bora la utalii duniani
Hata hivyo, Agosti mwaka jana, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) ilitangaza tozo mbalimbali zinazotozwa kwenye hifadhi inazosimamia nchini kwa wageni wa ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2019/2020.
Uchambuzi wa tozo hizo uliofanywa na Nukta (www.nukta.co.tz) umebaini kuwa tozo hizo zinawabeba zaidi wazawa kuliko wageni, jambo linawapa fursa zaidi ya kufaidika na rasilimali zao.
Licha ya kuwa tozo hizo zinatofautiana kulingana na hifadhi husika, bado tozo kwa wageni ziko juu kidogo ya zile wanazotozwa kulipa wazawa.
Mathalani, katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti, watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano wanaingia bure. Mgeni aliye juu ya miaka 15 itabidi agharamie Sh138,198 huku yule aliye na miaka chini ya 15 akitakiwa kugharamia Sh46,066 tu.
Kwa Watanzania, wakazi wa nchi za Afrika Mashariki na wataalamu, wanatozwa Sh69,099 kwa wote wenye miaka zaidi ya 15 na kwa wale wenye miaka mitano hadi 15 watatakiwa kulipa Sh23,033 kwa kila mtu.
Utalii umekuwa miongoni mwa sekta muhimu zinazotegemewa kuliingizia Taifa mapato na kukuza shughuli za uchumi.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018, mapato yaliyotokana na utalii yaliongezeka kwa asilimia 10.6 kutoka dola za Marekani milioni 2,199.8 mwaka 2017 hadi dola za Marekani milioni 2,432.9 mwaka juzi.