October 6, 2024

Majaliwa aeleza sababu za kumfukuza kazi kigogo wa ALAT

Ni Abraham Shamumoyo ambaye anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi ikiwemo fedha za jumuiya hiyo kutunzwa katika akaunti binafsi.

  • Ni Abraham Shamumoyo ambaye anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi ikiwemo fedha za jumuiya hiyo kutunzwa katika akaunti binafsi. 
  • Inadaiwa alikuwa anafanya maamuzi bila kushirikisha kamati ya utendaji ya jumuiya hiyo. 
  • Nafasi yake ilichukuliwa na na Elirehema Kaaya Juni mwaka huu. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameeleza Serikali iliamua kumuondoa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) , Abraham Shamumoyo kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi ikiwemo fedha za jumuiya hiyo kutunzwa katika akaunti binafsi. 

Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo (Julai 23, 2019) katika mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) unaoendelea jijini Mwanza, amesema utendaji wa Shamumoyo ulikuwa mbovu na wakati mwingine alikuwa anafanya maamuzi bila kushirikisha kamati ya utendaji ya taasisi hiyo. 

“Kuna maamuzi alikuwa akiyafanya bila kuishirikisha Kamati ya Utendaji. Kuna mikataba ilikuwa ikifanyika na mingine inahusisha hadi mataifa ya nje. Kuna fedha zilitolewa, zikawekwa kwenye akaunti binafsi na siyo akaunti ya ALAT,” amesema Majaliwa. 


Zinazohusiana: 


Amesema ALAT ni taasisi kubwa ya Serikali ambayo inahitaji kuheshimiwa, na siyo kuacha iendeshwe na mtu mmoja kama atakavyo.

 “ALAT ni taasisi kubwa na Serikali inaitegemea. Niwahakikishie kuwa Mheshimiwa Rais, anawathamini, anawapenda na anataka mchape kazi kuisaidia Serikali yenu,” amesema.

Hata hivyo, haijafahamika bayana ni lini Shamumoyo aliondolewa katika nafasi hiyo licha ya kuwa alikuwa  katika nafasi hiyo tangu mwaka 2015 ambapo Juni mwaka huu, Elirehema Kaaya aliteuliwa kuchukua nafasi yake.