October 7, 2024

Majaliwa aiomba Cuba kuongeza uzalishaji wa sukari Tanzania

Amewakaribisha wawekezaji wa nchi hiyo kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kuboresha kilimo cha miwa na kuanzisha viwanda vya sukari.

  • Amesema nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari duniani. 
  • Amewakaribisha wawekezaji wa nchi hiyo kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kuboresha kilimo cha miwa na kuanzisha viwanda vya sukari.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Cuba kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha kilimo cha miwa na kuongeza uzalishaji wa sukari ili kukabiliana na changamoto ya kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi. 

Majaliwa ametoa ukaribisho huo leo (Septemba 9, 2019) jijini Dodoma wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez.

 Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa amesema Serikali ya Cuba imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa sukari, hivyo amewakaribisha Wacuba waje nchini washirikiane na Serikali ya Tanzania katika kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kuboresha kilimo cha miwa na kuanzisha viwanda vya sukari.

 Pia, Waziri Mkuu amewakaribisha wawekezaji kutoka Cuba wawekeze katika sekta ya utalii wa fukwe kwa sababu Tanzania ina fukwe nzuri.

 Akitolea mfano wa  mji mmoja wa Varadero wa nchini Cuba unaingiza watalii zaidi ya milioni moja kwa mwaka na unategemea kivutio kikubwa kimoja tu cha fukwe ambayo ina urefu wa kilomita 22.


Zinazohusiana: 


 Amekutana na kiongozi huyo leo (Jumatatu, Septemba 9, 2019) ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma. Waziri Mkuu ameishukuruSerikali ya Cuba kwa ushirikiano mzuri inaoutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kuboresha maendeleo ya jamii.

 Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati yake na Serikali ya Cuba kwa kuwa nchi hiyo ni mojawapo kati ya nchi zenye ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania katika masuala ya kisiasa, kijamii, kiafya na kiuchumi.

 “Tanzania na Cuba zina uhusiano wa kihistoria. Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati nchi zote mbili, yaliyokuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere na Rais wa zamani wa Cuba, hayati Fidel Castro.

Mfano katika sekta ya afya, madaktari wengi kutoka Cuba wamekuwa wakija Tanzania kutibu wagonjwa waliokuwa na maradhi makubwa na pia Serikali ya Cuba imekuwa ikitoa fursa kwa Watanzania kwenda kusomea fani ya udaktari,” amesema Majawali. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akipokea zawadi ya kitabu cha Rais wa kwanza wa Cuba, Fidel Castro, kutoka kwa Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez, kwenye ukumbi wa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Septemba 9.2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Naye Gonzalez amesema Serikali ya Cuba itahakikisha uhusiano wake na Serikali ya Tanzania unakuwa endelevu huku akipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo pamoja na kukuza uchumi.

Amesema Cuba imefurahishwa na Tanzania kufungua ofisi ya ubalozi nchini Cuba kwa sababu imezidi kuimarisha mahusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili. 

Kiongozi huyo pia amefanya ziara katika visiwa vya Zanzibar kabla ya kwenda Dodoma.