July 5, 2024

Majaliwa ataka viwango vya ubora miradi ya maendeleo Tanzania

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aagiza isimamiwe vizuri ili kuhakikisha inakuwa na viwango vinavyoendana na thamani ya fedha.

  • Aagiza isimamiwe vizuri ili kuhakikisha inakuwa na viwango vinavyoendana na thamani ya fedha.
  • Atolea mfano uwanja wa ndege wa Songea ulivyoboreshwa kwa kuzingatia viwango vya ubora. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema miradi yote inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania lazima isimamiwe vizuri ili kuhakikisha inakuwa na viwango vinavyoendana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo Januari 6, 2021 alipozungumza na viongozi wa mkoa wa Ruvuma katika uwanja wa ndege wa Songea akiwa njiani kuelekea Dar es Salaam. 

“Maelekezo ya Serikali kwenye maeneo yote muhimu ya miradi isimamiwe kwa kina na hasa thamani ya fedha na viwango vya ujenzi wa miradi yenyewe,” amesema Majaliwa. 

Amesema watendaji wa Serikali wanapaswa kusimamia miradi yote inayotekelezwa ili iendane na thamani ya fedha inazotoa kama ilivyo kwa baadhi ya miradi iliyojengwa mkoani Ruvuma.

“Tumeona Sekondari ya Tunduru, majengo ya halmashauri ya wilaya ya Mbinga, barabara ya Mbinga-Mbamba Bay na uwanja wa ndege utaalamu umetumika na thamani ya fedha ipo,” amesisitiza Waziri Mkuu.


Zinazohusiana: 


Kwa sasa, uwanja wa ndege wa Songea unakarabatiwa ili kuimarisha huduma za usafiri wa anga mkoani humo na zaidi ya Sh37 bilioni zimetumika kuimarisha uwanja huo.

Ukarabati huo umehusisha njia ya kurukia ndege yenye uwezo wa kupokea abiria zaidi ya 150, jengo la abiria na maeneo ya maegesho yenye uwezo wa kuegesha ndege kubwa sita. 

Uwanja huo utakapokamilika utaruhusu ndege kutua usiku na mchana, jambo litakalofungua fursa mbalimbali za biashara katika mkoa huo wa kusini mwa Tanzania.