October 6, 2024

Majaliwa atoa maagizo mazito mradi wa nyumba za NSSF Kigamboni

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema nyumba zote zinazojengwa na taasisi za Umma katika wilaya Kigamboni jijini Dar es salaam zikiwemo za Mfuko wa Hifadhi kamili ya Jamii (NSSF) zinapaswa kukamilika haraka ili ziuzwe ua kupangishwa ili kuwapa ahueni wananc

  • Aagiza ujenzi wake ukamilike haraka ili ziuzwe au kupangishwa.
  • Aagiza NSSF kuweka miundombinu yote ili kuvutia wateja.
  • Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam nao wapewa majukumu yake.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema nyumba zote zinazojengwa na taasisi za Umma katika wilaya Kigamboni jijini Dar es salaam zikiwemo za Mfuko wa Hifadhi kamili ya Jamii (NSSF) zinapaswa kukamilika haraka ili ziuzwe ua kupangishwa ili kuwapa ahueni wananchi wa mkoa huo.

 Majaliwa ametoa maagizo hayo Novemba 27, 2019 baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa nyumba za Mfuko wa Hifadhi kamili ya Jamii (NSSF), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Watumishi Housing iliyopo katika wilaya ya Kigamboni.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu jana, inaeleza kuwa  inasikitisha kuona kwamba watumishi wa umma na wananchi  jijini Dar es Salaam hawana nyumba nzuri za kuishi wakati zipo nyumba nyingi  nzuri zimejengwa na zinahitaji umaliziaji mdogo tu ili ziweze kukalika.

 Majaliwa ameitaka menejimenti ya NSSF kakamilisha haraka ujenzi na uwekaji wa miundombinu ya umeme, maji safi na maji taka  katika nyumba zake 161 zilizoko  Tuangoma, 820 zilizoko Mtoni Kijichi na 439 zilizoko Dungu ili ziuzwe na kuepusha uwezekano wa uharibifu unaoweza kutokea  kwa nyumba hizo kakaa muda mrefu bila kupata wanunuzi au wapangaji.

 Ili kufanikisha jambo hilo, Majaliwa amemtaka Mthamini Mkuu wa Serikali atathmini nyumba hizo na kutoa   bei halisi ya soko kwa sasa ili kuwawezesha Watanzania wengi na hasa watumishi wa umma kununua na kupanga katika nyumba hizo.

 Pia, Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa wilaya  na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Kigamboni kuwasaidia watumishi wa wilaya na Halmashauri hiyo  kuingia mikataba rafiki itakayowawezesha watumishi  hao kupewa kipaumbele katika kununua au kupanga kwenye nyumba hizo.


Zinazohusiana: 


Wanafunzi vyuoni nao wakumbukwa nyumba za NSSF 

Katika hatua, nyingine, Majaliwa ameitaka Menejimenti ya NSSF kufikiria namna ya kuzungumza na viongozi wa vyuo mabalimbali kama vile Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Mwalimu Nyerere ili wanafunzi wa vyuo hivyo wapatiwe fursa ya kupanga katika nyumba hizo kwa bei watakazomudu. 

Pia Mheshimiwa Majaliwa ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es salaam ukishirikiana na Mamlaka ya usafiri wa Nchi kavu na majini (SUMATRA) kuanzisha njia za mabasi ya daladala  zitakazoanzia au kupitia kwenye nyumba za NSSF Mtoni Kijichi na Dungu ili kuwezesha wapangaji na wananchi watakaonunua nyumba hizo kupata usafiri wa umma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mradi wa nyumba za NSSF, zilizopo Tuangoma katika Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam, Novemba 27, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Vilevile, Waziri Mkuu ameuagiaza uongozi huo kuhakikisha kwamba eneo la Mtoni Kijichi zilipojengwa nyumba za NSSF na NHC linapata huduma za Shule, Kituo cha Afya na Kituo cha Polisi kwani litakuwa na wakazi wengi .

Ili kuongeza thamani ya nyumba hizo na kuvutia wapangaji na wanunuzi, NSSF imetakiwa kuboresha barabara kwenye mitaa yote zilipojengwa nyumba hizo kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

 “Nashauri ziwekwe taa za sola kwenye barabara za mitaa yote ya nyumba hizi ili kupendezesha eneo na kuwafanya wananchi wahamasike kununua na kuishi katika nyumba hizi,” amesema Majaliwa.

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema wizara yake imeyapokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu na kwamba watafanya kila njia ili kuhakikisha kwamba majengo yote yanakamilika haraka na kuuzwa au kupangishwa.