October 6, 2024

Majaliwa atoa maagizo mazito TCU

Ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) itafute njia bora ya kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili kuondoa mtazamo hasi kwenye jamii kuwa kazi kubwa ya tume hiyo ni kuvifungia vyuo vikuu

  • Ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) itafute njia bora ya kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi.
  • Pia yatakiwa kuondoa mtazamo hasi kwenye jamii kuwa kazi kubwa ya TCU ni kuvifungia vyuo vikuu.
  • Amesisitiza kwamba hakuna mbadala wa elimu bora.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) itafute mbinu bora zaidi ya kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili  kuondoa taswira hasi miongoni mwa jamii kuwa kazi kubwa ya tume hiyo ni kuvifungia vyuo hivyo. 

Waziri Mkuu aliyekuwa akizungumza leo (Julai 17, 2019) wakati akifungua maonyesho ya 14 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, amesema TCU ivisaidie vyuo vikuu kufikia viwango vinavyotakiwa na siyo kuwapunguzia viwango vya matakwa ya usajili.

“Ni wakati muafaka kwa tume kujipambanua kwenye uwezeshaji na ushauri ili kuondoa taswira hasi miongoni mwa jamii kwamba kazi kubwa ya TCU ni kuvifungia vyuo vikuu badala ya kuvisaidia kutatua changamoto zinazovikabili,” amesema.

Amesema Serikali inatambua kwamba vyuo vikuu binafsi ni washirika muhimu wa maendeleo ya sekta ndogo ya elimu ya juu nchini. 


Zinazohusiana: 


Akizungumzia idadi ndogo ya wahitimu wa elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema takwimu za kimataifa za ushiriki wa elimu ya juu zinaonesha kuwa hadi kufikia mwaka 2017 ni asilimia moja hadi tatu tu ya Watanzania au Watanzania watatu  kwa kila 100 wenye umri chini ya miaka 25 wanapata elimu ya chuo kikuu.

“Idadi hii ni ndogo zaidi ya majirani zetu wa Kenya wenye asilimia nne, Zambia asilimia nne na Namibia asilimia 14. Bado tunayo kazi kubwa sana ya kufanya. Natoa maelekezo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iongeze jitihada na mikakati ya kuboresha uwiano huu ambao upo chini ikilinganishwa na majirani zetu,” amesisitiza.

Amesema ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata nafasi ya elimu ya juu, ni lazima tupange mikakati kama nchi kwa kushirikiana na sekta binafsi, ambao ni wadau wakubwa katika elimu ya juu. 

“Taarifa nilizonazo ni kwamba, kati ya wahitimu wote wa vyuo vikuu kwa mwaka, asilimia 25 wanatoka katika vyuo vikuu binafsi. Mchango huu si mdogo, na ningetamani uongezeke zaidi,” amesema.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia mashine ya kutayarishia vitambulisho vya Taifa, wakati akikagua banda la (NIDA), kwenye ufunguzi wa Maonesho ya 14 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es salaam, Julai 17.2019. Kulia ni Mtaalamu wa mashine hiyo, Marwa Mbolea. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewapa changamoto wakuu wa vyuo vikuu nchini wabadilishe mtazamo wao juu ya upimaji wa ufanisi wa wahitimu na badala yake upimaji wao ujielekeze kwenye kutoa suluhisho na kubadilisha maisha ya Watanzania badala ya kutumia machapisho ya kitaaluma.

Matarajio ya Serikali ni kuona kwamba tafiti na vipimo vya ufanisi kwenye vyuo vikuu viwe vinatoa bidhaa mbalimbali za kuleta ajira pamoja na kukabiliana na matatizo ya kijamii.

Mwenyekiti wa TCU, Prof Jacob Mtabaji amesema kuna uhaba wa wahadhiri wenye sifa stahiki katika vyuo vikuu vingi na akawaomba wakuu wa vyuo hivyo wawasomeshe wahadhiri katika ngazi mbalimbali ili wakirudi wajiunge na vyuo husika.

Taasisi 81 za elimu ya juu zimeshiriki maonesho hayo ambapo taasisi 15 ni za nje ya nchi na taasisi 66 ni za hapa nchini ambapo yatafungwa Julai 20, mwaka huu.