October 8, 2024

Majaliwa atoa maagizo Wizara ya Kilimo malipo ya korosho

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe kuwa asilimia tatu ya wakulima wa zao la korosho ambao hawajapata fedha zao wahakikiwe na kulipwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Naibu Waziri Wizara ya Kilimo, Wakuu wa Wilaya wa Mkoa wa Lindi na Mtwara, Mkatibu Tawala wa Mikoa hiyo, Wakurugenzi  wa Benki ya TADB na CPB, katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, kabla ya kikao na Wafanyabiashara wa korosho wa Mikoa hiyo, Januari 3, 2020. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Ameitaka ihakikishe asilimia tatu ya wakulima wa zao la korosho waliosalia wanahakikiwa na kulipwa.
  • Wakulima wametakiwa kuendelea kuwa na subira na kwamba haki yao itapatikana.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe kuwa asilimia tatu ya wakulima wa zao la korosho ambao hawajapata fedha zao wahakikiwe na kulipwa.

Hadi sasa, takriban asilimia 97 ya wakulima wa korosho waliouza korosho zao katika msimu wa 2018/2019 wameshahakikiwa na kulipwa.

Majaliwa ametoa maagizo hayo jana (Januari 3, 2020) alipokutana na baadhi ya wakulima wa korosho kutoka wilaya za Ruangwa, Masasi na Tandahimba, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima hao huku akiwataka waendelee kuwa na subira na kwamba haki yao itapatikana.

 “Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli ipo makini, hivyo hakuna Mtanzania yeyote atakayepoteza haki yake,” amesema Majaliwa.

Korosho ina upekee wake katika maisha ya Watanzania hasa wakulima wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, Ruvuma na Tanga kwa kuwa hutegemea zao hilo kujiingizia kipato ambacho hutumika kutunza familia na kusomesha watoto ili kuondokana na umaskini katika jamii.

Lakini kupitia korosho wanalipa ushuru na kodi kwa Serikali ili kuboresha huduma za kijamii kama elimu na afya katika maeneo yao. 


Zinazohusiana:


Kwa upande wao, wakulima wameishukuru Serikali kwa kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi na kwamba wanaimani ya kulipwa madai yao.

Mmoja wa wakulima hao, Mariamu Mganda amesema anamshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuwasikiliza kwani wamepata tumaini la kulipwa fedha zao.

Mkulima Mwingine Abdulkareem Said amesema ameridhishwa na utendaji kazi wa Serikali hususan baada ya Waziri Mkuu kukubali kusikiliza kero zao.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wanachama wa vyama vya ushirika pale watakapoona ushirika wao hauendi vizuri wasisite kutoa taarifa Serikalini.

Amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya wawachukulie hatua viongozi wote wa vyama vya ushirika watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.