November 24, 2024

Majaliwa awabana watendaji Singida matumizi mabaya fedha za umma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa asema Serikali iko macho wakati wote na itamfikia na kumchukulia hatua kila mtumishi wa umma anayetumia vibaya fedha za Serikali.

  • Baadhi yao waonywa, wasimamishwa kwa matumizi mabaya ya ofisi ikiwemo ubadhirifu wa fedha.
  • Takukuru mkoani Singida yapewa rungu kuwachunguza watendaji wasio waaminifu.
  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa asema Serikali iko macho wakati wote. 

Dar es Salaam. Ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mkoani Singida imeendelea kuwaweka katika wakati mgumu watumishi wa umma mkoani humo huku wengine wakisimamishwa na kuchunguzwa kutokana na matumizi mabaya ya fedha za Serikali.

Jana jioni (Oktoba 6, 2019), Majaliwa alimwagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Singida, Adili Elinipenda amkamate Afisa Manunuzi wa Chuo cha Ualimu Kinampanda, Francis Muyombo kwa kukiuka taratibu za manunuzi ya Serikali na kughushi nyaraka. 

Pia alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, ACP Sweetbert Njewike amkamate na kumhoji Joseph Kisaka ambaye alikuwa mzabuni wa chuo hicho kwa kukiuzia chuo vifaa vilivyo chini ya kiwango.

Alitoa maagizo hayo jana jioni, wakati akikagua ukarabati wa majengo ya chuo hicho kilichopo wilayani Iramba, mkoani Singida ambako alibaini “delivery note” (maelezo ya utoaji) ikionyesha kitasa kimoja kimenunuliwa kwa  Sh70,000 badala ya Sh25,000.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hati ya manunuzi inaonyesha chuo kilipaswa kununua vitasa ambavyo vinafunga mara tatu (vya 3-level) lakini alipokwenda kukagua milango kwenye mabweni, ukumbi, na bwalo alikuta ni vitasa vya kufunga mara moja (vya 1-leavel).

Alipoulizwa wametumia utaratibu gani kununua vifaa hivyo, Mkuu wa Chuo hicho, Hamisi Njau alisema walikuwa wakitumia kamati ya manunuzi ambayo mwenyekiti wake alikuwa ni Makamu Mkuu wa Chuo na Katibu wake ni Afisa Manunuzi, Muyombo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa ameshika kipande cha tofali, kilichobomoka, wakati akikagua kituo cha afya cha Ndago, wilayani Iramba, katika Mkoa wa Singida, na kutoridhishwa na ujenzi wa kituo hicho, Oktoba 6.2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Jana hiyo hiyo, Majaliwa alimwagiza Elinipenda achunguze watumishi 48 waliojihusisha na upotevu wa fedha kwa njia za udanganyifu ikiwemo upotevu wa makusanyo ya ndani kupitia mawakala wa ukusanyaji mapato (POS) ambapo mawakala wanaokusanya fedha wanashirikiana na watumishi wa halmashauri na kuzitumia bila kuziingiza benki.

“Kuna kundi la watumishi 10 wakiongozwa na mtu wa Tehama, wameshirikiana kupata password na fedha zikishakusanywa wanazitoa na kuzitumia bila kuzipelekea benki. Wamesahau kwamba malipo yalipoingizwa mara ya kwanza, data ilirekodiwa kwenye mfumo wa malipo na sisi tunaona ni kiasi gani kimekusanywa,” amesema Majaliwa. 

Watumishi hao ni Salum Omari (Mtaalamu wa Tehama); Adam Mzengi (Mhasibu kahamishiwa Gairo); Rafaeli Nasari; Caroline Makundi (kahamishiwa Singida Manispaa), Edson Ally (Afisa Biashara); na Martin Kimisho (Mhasibu Msaidizi).

Wengine ni Prosper Banzi (Afisa Biashara); Hassan Ponda (Mhasibu kituo cha afya Ndago); Hafidh Ngayunda (Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya) na Muhidin Mohammed (Mweka Hazina wa Wilaya) ambaye tayari amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma hizo.

Kutokana na upotevu huo, Waziri Mkuu ameagiza Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya akae pembeni hadi uchunguzi wa Takukuru utakapokamilika.

Akibainisha mchezo mwingine uliochezwa na watumishi wa Halmashauri hiyo, Majaliwa amesema kuna watumishi 38 ambao walilipwa Sh46 milioni ambazo zilikuwa sehemu ya Sh400 milioni za kujenga vituo vya afya vya Ndago na Kinampanda wilayani humo.


Zinazohusiana: 


DED Mkalama achunguzwa

Jumamosi ya Oktoba 5, 2019 Majaliwa alimwagiza Kamanda wa Takukuru mkoa wa Singida, Elinipenda amchunguze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama, Godfrey Sanga kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Baadhi ya tuhuma alizonazo ni kujilipa posho ya safari Machi mwaka huu bila kusafiri, kuwasainisha watumishi wa chini yake vocha na kisha kuwapa ‘asante kidogo’ kwa madai fedha hizo zinaenda mkoani, kujilipa stahiki kabla ya wakati na kuagiza gari liende gereji kwa matengenezo bila nyaraka zozote.

“Kuna watumishi wanne uliwaambia wasaini vocha ya Sh1.32 milioni. Hii ni kwa safari iliyopangwa kati ya tarehe 15 na 24 Septemba, mwaka huu; ukawapa asante ya Sh30,000 ukidai kuwa zinatakiwa mkoani. RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) ni kweli hela hiyo ililetwa mkoani?,” alihoji Majaliwa na kujibiwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Dk Anjelina Lutambi ambaye alikanusha kutoa maagizo. 

Waziri Mkuu yupo mkoani Singida kwa ziara ya kikazi  ya siku nne ambayo ilianza Oktoba 4, ikiwa ni hatua ya kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo mkoani humo.