October 6, 2024

Majaliwa awakalia kooni wakurugenzi wawili skimu ya umwagiliaji Narunyu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, wafike ofisini kwake Dar es Salaam kesho asubuhi na taarifa kuhusu kusua sua kwa skimu ya umwagiliaji ya Narunyu.

  • Amewaagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, wafike ofisini kwake Dar es Salaam kesho asubuhi.
  • Wanatakiwa kutoa taarifa ya fedha zilizobakia zaidi ya Sh240 milioni za mradi wa skimu hiyo.
  • Mradi huo umekuwa ukisua sua kwa muda mrefu. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, wafike ofisini kwake Dar es Salaam kesho asubuhi na taarifa kuhusu kusua sua kwa skimu ya umwagiliaji ya Narunyu.

Ametoa agizo hilo, baada ya kufika eneo la mradi leo mchana (Oktoba 17, 2019) na kupokea malalamiko ya wanajumuiya ya umwagiliaji kutoka kwa Mwenyekiti wao, Bakari Awadhi juu ya kusuasua kwa mradi huo na kukosa majibu ya kuridhisha juu ya mradi huo.

“Nilitarajia niwakute hapa Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Umwagiliaji wa Wilaya na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda. Nimeagiza wanikute uwanja wa ndege Lindi au Dar es Salaam na kesho asubuhi waje ofisini kwangu wanipe taarifa kamili ya mradi huu. Nataka nijue fedha zilizobakia zaidi ya Sh240 milioni ziko wapi,” amesema Majaliwa.

Amesema kama watendaji wawili hao watashindwa kufika kesho ofisini kwake, anaweza kufanya maamuzi mengine. 

“Walipaswa niwakute hapa wananisubiri kwa sababu nilitoa taarifa tangu jana kwamba nitapita hapa. Nimepata taarifa kwamba wamesafiri kutoka Mtwara na leo asubuhi walikuwepo Lindi mjini. Waje ofisini kesho, wakishindwa, nitachukua maamuzi mengine,” amesema.

Hata wakati Waziri Mkuu amefika uwanja wa ndege wa Lindi, maafisa hao walikuwa hawajafika kwa sababu simu zao hazikupatikana, na akaagiza waje Dar es Salaam kesho asubuhi. 


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, mradi huo ni wa muhimu kwa sababu unatiririsha maji wakati wote. 

Majaliwa amesema kutokana na umuhimu wa mradi huo, hivi sasa wangekuwa wanazalisha mazao ya kila aina na kusema “hapa ni mahali pa kuzalisha mazao mengi, leo unalima mahindi, ukivuna unapanda matikiti, ukitoa unapanda nyanya. Sasa nitapasimamia mwenyewe.”

Amewataka wanaushirika wanaounda jumuiya ya umwagiliaji wahakikishe kila mmoja anatambua eneo lake na mara kazi ikianza wawe tayari kuanza kilimo. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua skimu ya umwagiliaji ya Kiwalala katika Halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi, Oktoba 17, 2019. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga na wa tatu kushoto ni Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mapema, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga alimweleza Waziri Mkuu kuwa katika mafaili aliyoyapitia ofisini kwake alibaini kwamba mradi huo ulitengewa Sh788 milioni  ambapo mkandarasi wa kwanza kutoka kampuni ya Chest Investments alilipwa Sh121 milioni lakini akashindwa kazi.

“Mkandarasi wa pili ambaye ni D & L naye alilipwa zaidi ya Sh400 milioni naye pia akashindwa kazi ya kuondoka tope. Kwenye ripoti, inaonesha zilibakia Sh249 milioni,” amesema Ndemanga. 

Naye Mwenyekiti wa wanajumuiya ya umwagiliaji ya Narunyu, Bakari Awadhi alisema skimu hiyo yenye ukubwa hekta 1,200 imekuwa ikijaa maji na kufunika mitaro na hatimaye kujaa mchanga.

Alimwomba Waziri Mkuu awasaidie kuifufua skimu hiyo kwa sababu inawanufaisha wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.