October 6, 2024

Majaliwa awakaribisha wawekezaji kutoka Vietnam kujenga viwanda

Amesema viwanda hivyo vitakuwa vinatumia malighafi za kilimo ili kuwafaidisha wakulima wa Tanzania.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Vietnam nchini Tanzania, Nguyen  Doanh, ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam, Julai 3, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Amesema viwanda hivyo vitakuwa vinatumia malighafi za kilimo ili kuwafaidisha wakulima wa Tanzania.
  • Wafanyabiashara wa Vietnam nao wakaribishwa kununua korosho na kahawa ya Tanzania. 
  • Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Trinh Dinh Dung kuingia Tanzania wiki ijayo. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchi ya Vietnam waje Tanzania kuwekeza katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za kilimo ili wakulima wapate soko la uhakika la mazao yao.

Amesema Serikali imeanzisha Wizara ya Uwekezaji iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kuifanya Tanzania kuwa ni mahali bora na salama kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Majaliwa ametoa wito huo leo (Julai 3, 2019) wakati akizungumza na Balozi wa Vitemam nchini Tanzania, Nguyen Doanh ofisini kwake, Magogoni jijini Dar Es salaam. 

“Serikali imeendelea kuondoa  vikwazo vya  kuanzisha na kuendesha  biashara  kwa kupitia upya   sheria, kanuni na taratibu za biashara  na kuzifuta zile  ambazo zimethibitika  kuwa zinayafanya mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kuwa magumu,” amesema Majaliwa. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Vietnam imepiga hatua kubwa katika ujenzi na uendeshaji wa viwanda vya nguo, Tanzania ingefurahi kuona viwanda vya aina hiyo vinajengwa hapa nchini na wawekezaji wa nchi hiyo.

Amesema kuwa ununuzi wa mazao ya kilimo kama vile pamba, korosho, kahawa na tumbaku ni fursa nyingine ya kibiashara ambayo wafanyabiashara wa Vietnam wanakaribishwa kuichangamkia ili wanufaike na mazao hayo.


Zinazohusiana:


Tanzania na Vietnum zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya mawasiliano ambapo nchi hiyo ina kampuni ya simu za mkononi ya Halotel inayoendesha shughuli zake nchini. 

Balozi Doanh ametumia fursa hiyo kumweleza Waziri Mkuu juu wa ujio wa Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Trinh Dinh Dung anayetarajiwa kufanya ziara yake ya kikazi nchini kuanzia Julai 9 hadi 11 mwaka huu. 

Amesema Dung huyo anatarajiwa kuambatana na wafanyabiashara wasiopungua 20 kutoka kampuni kubwa za nchini Vietnam.

Nchi za Vietnam na Tanzania zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1965. Mwaka 1984, Vietnam ilifunga ofisi ya Ubalozi  wake hapa nchini kwa muda na kuufungua upya mwaka 2003.