November 24, 2024

Majaliwa awapa mtihani wanaotaka uchumi wa kati 2025

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ili Tanzania ifikie lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025 inayoongozwa na uchumi wa viwanda, haina budi kutimiza vigezo mbalimbali ikiwemo cha ukuaji wa uchumi kwa kiwango cha asilimia 12 kwa mwaka.

  • Awataka kutimiza vigezo mbalimbali ikiwemo cha ukuaji wa uchumi kwa kiwango cha asilimia 12 kwa mwaka.
  • Awataka kutafakari mbinu mpya za kufikia vigezo hivyo muhimu vya kuijenga Tanzania mpya ya viwanda.
  • Asema mpaka sasa, viwanda vipya zaidi ya 4,000 vimejengwa nchini na kuajiri Watanzania 306,180. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ili Tanzania ifikie lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025 inayoongozwa na uchumi wa viwanda, haina budi kutimiza vigezo mbalimbali ikiwemo cha ukuaji wa uchumi kwa kiwango cha asilimia 12 kwa mwaka.

Amesema vigezo vingine ni mchango wa viwanda katika Pato la Taifa usiopungua asilimia 15; utoaji ajira rasmi na za moja kwa moja uongezeke na kufikia asilimia 40 ya ajira zote; na sekta ya viwanda iweze kuiingizia nchi mapato ya fedha za kigeni zaidi ya asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni.

“Ili kufikia vigezo hivyo na kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya viwanda, ni lazima tujizatiti na kuimarisha ushirikiano wa karibu baina ya sekta ya umma na sekta binafsi,” amesema Majaliwa jana usiku (Oktoba 17, 2019) wakati akizungumza katika Tuzo za Rais kwa Wazalishaji Bora wa mwaka 2018 iliyofanyika katika hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Amewataka washiriki katika hafla hiyo waitumie fursa ya kutafakari mbinu mpya za kufikia vigezo hivyo muhimu vya kuijenga Tanzania mpya ya viwanda.

“Kila mmoja wetu anatambua umuhimu wa sekta ya viwanda katika kukuza uchumi wa nchi yoyote duniani. Viwanda ndivyo vimekuwa chimbuko la maendeleo ya haraka ya nchi mbalimbali duniani na mhimili mkuu wa kutegemewa katika kuondoa umasikini kwa kutoa ajira nyingi na za uhakika kwa wananchi,” amesema Majaliwa katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.


Zinazohusiana:


Amesema takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2018, sekta ya viwanda imetoa ajira rasmi 306,180 ikilinganishwa na ajira 280,899 za mwaka 2017; sawa na ongezeko la asilimia tisa. 

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki ili kuwezesha sekta ya viwanda kukua kwa haraka na kutoa mchango mkubwa zaidi katika Pato la Taifa na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini wa wananchi. 

Amesema mpaka sasa, viwanda vipya zaidi ya 4,000 vimejengwa katika mikoa mbalimbali nchini.

 “Viwanda vilivyojengwa vinazalisha bidhaa za ujenzi (saruji, nondo, vigae, mabomba, marumaru, n.k); pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ikiwemo nafaka, matunda, mafuta ya kupikia na bidhaa za ngozi,” amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi tuzo ya ushindi wa jumla, Satbir Singh Hanspaul ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya HANSPAUL katika utoaji wa tuzo za Rais kwa viwanda vilivyofanya vizuri kwa mwaka 2018 kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam, Oktoba 17, 2019. Watatu kushoto ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa na Kushoto ni Mwenyekiti wa  Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Subhash Patel. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Akizungumza na washiriki wa hafla hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amesema wizara yake kwa kushirikiana na sekta binafsi itaendelea kuondoa kero zinazokwamisha ufanisi na ukuaji wa sekta ya viwanda. 

Amezitaja baadhi ya kero hizo kuwa ni ucheleweshaji wa malipo ya madai ya kodi za ongezeko la thamani (VAT) na asilimia 15 ya ziada inayolipwa na waagizaji wa sukari ya viwandani; ushindani usio na uwiano na bidhaa za bei nafuu kutoka nje ya nchi kama vile nondo, mabomba ya plastiki, nguo na mavazi, bidhaa za ngozi na marumaru.