October 8, 2024

Majaliwa awapa rungu watoto wanaokatishwa masomo Tanzania

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inawataka watoto watoe taarifa za watu wanaotaka kuwakatisha masomo yao kwa viongozi wa vijiji waliopo kwenye maeneo yao ili hatua za kisheria zichukuliwe.

  • Awataka watoe taarifa za watu wanaotaka kuwakatisha masomo yao kwa viongozi wa vijiji.
  • Awaagiza wakuu wa mikoa, wilaya kuwachukulia hatua wote watakaowakatisha masomo yao. 
  •  Vijana watakiwa kujihadhari na watoto wa shule, wakikutwa nao jela miaka 30. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inawataka  watoto hasa wa kike watoe taarifa za watu wanaotaka kuwakatisha masomo yao kwa viongozi  wa vijiji waliopo kwenye maeneo yao ili hatua za kisheria zichukuliwe. 

Majaliwa ametoa agizo hilo jana (Januari 19, 2020) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo cha Mafunzo ya Amali cha Daya kilichopo Mtambwe wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba.

Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kuwalinda watoto wa kike, lengo likiwa ni kuhakikisha wanamaliza masomo yao na hatimaye waweze kujikwamua wao pamoja na familia zao.

Asema watoto wa kike wanatakiwa waheshimiwe na jamii kwa kuachwa waendelee na masomo bila ya usumbufu wowote na atakayebainika kukatisha masomo yao adhabu yake ni miaka 30 jela.

“Wanafunzi wa kike hakikisha mtu yeyote atakayekugusa, kukufuatilia nenda kamshtaki kwa kiongozi wa Shehiya (kijiji) husika. Vijana jihadharini na watoto wa shule ukikutwa naye jela miaka 30, “ amesisitiza Majaliwa katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu leo (Januari 20, 2020).


Zinazohusiana:


Aidha, amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini Tanzania wasimamie ipasavyo suala la elimu hususani kwa watoto wa kike na kuwachukulia hatua za kisheria watakaowakatisha masomo yao.

Awali, akisoma taarifa za ujenzi wa chuo hicho, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Madina Abdallah  amesema mpaka kukamilika kwake mradi huo utagharimu jumla ya dola za Marekani milioni 25.8 kati yake dola milioni 23.4 zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) huku dola milioni 2.4 zikitolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Amesema kwa mujibu wa mkataba wa mradi huo, kazi ya ujenzi inajumuisha vituo viwili vya Mafunzo ya Amali ambavyo ni Makunduchi Unguja na Daya Pemba.

Pia upanuzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Utalii Maruhubi na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume pamoja na ununuzi wa vifaa vya kufundishia.