October 6, 2024

Majaliwa awasilisha ombi la mafunzo kwa madaktari bingwa Japan

Ameiomba Serikali ya Japan ikubali kutoa mafunzo zaidi kwa madaktari bingwa wa upasuaji na wa magonjwa ya figo na moyo kutoka Tanzania.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mshauri  Maalum  wa masuala ya afya  wa taasisi ya Tokushukai General Incorporated ambayo  iko chini ya serikali ya Japan, Akio Egawa  kwenye uwanja wa ndege wa Narita nchini Japan kabla ya kuondoka kurejea nyumbani baada ya kukamilisha ziara yake ya kikazi nchini humo, Septemba 2, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Ameiomba Serikali ya Japan ikubali kutoa mafunzo zaidi kwa madaktari bingwa wa upasuaji na wa magonjwa ya figo na moyo kutoka Tanzania.
  • Amesema hatua hiyo itasaidia kukidhi mahitaji ya madaktari hao katika hospitali za Tanzania. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiomba Serikali ya Japan ikubali kutoa mafunzo zaidi kwa madaktari bingwa wa upasuaji na wa magonjwa ya figo na moyo kutoka Tanzania ili kukidhi mahitaji ya madaktari hao nchini.

Waziri Mkuu amewasilisha ombi hilo jana (Septemba 2, 2019) wakati alipozungumza na Mshauri Maalum wa masuala ya afya wa taasisi ya Tokushukai General Incorporated Association iliyo chini ya Serikali ya Japan, Akio Egawa kwenye uwanja wa ndege wa Narita nchini Japan akiwa njiani kurejea Tanzania. 

“Nashauri uandaliwe utaratibu wa kubadilishana watalaam ili Watanzania waende Japan kutibu wagonjwa na Wajapan waje nchini kufanya kazi kwenye hospitali zetu lengo likiwa ni kubadilishana  ujuzi na kuongeza uzoefu,” amesema Majaliwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, hivi sasa Tanzania ni kimbilio kwa nchi jirani katika tiba ya moyo na figo, hivyo madaktari bingwa wa upasuaji na madaktari bingwa wa magonjwa hayo wanahitajika sana.

Amesema baada ya hospitali ya Benjamini Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma kufanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa saba chini ya ufadhili wa taasisi hiyo, nchi jirani pia zinategemea kupata huduma hiyo Tanzania, hivyo madaktari na vifaa tiba zaidi vinahitajika Ili kujenga uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wa ndani na nje.


Soma zaidi: Majaliwa aishawishi Toshiba kuwekeza Tanzania


Waziri Mkuu ameishukuru taasisi hiyo kwa misaada yake ambayo kwa kiwango kikubwa imefanikisha kuanzishwa kwa tiba ya upandikizaji figo katika hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

Pia, Waziri Mkuu amemkaribisha Tanzania Egawa kuona mwenyewe maeneo mengine ambayo taasisi   anayoiongoza inaweza kusaidia ili kuifanya nchi yetu kuwa na uwezo mkubwa katika tiba ya upandikizaji wa figo barani Afrika.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa Egawa ameishi Tanzania kwa miaka mitatu akifanya kazi kwenye ubalozi wa Japan uliopo Dar es Salaam, hivyo anaifahamu vizuri Tanzania na anajua umuhimu na mahitaji ya huduma za afya nchini na anafahamu mikakati Serikali kuhusu kuboresha huduma za afya.

Egawa amemwahidi Majaliwa kuwa taasisi yake iko tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania kuendelea kusaidia hospitali ya Benjamin Mkapa ili kuiimarisha na kuiwezesha kufanya vizuri zaidi katika huduma ya tiba ya figo na moyo. 

Katika ziara hiyo ya Japan, Majaliwa alimwakilisha Rais John Magufuli katika Mkutano wa Saba wa “Tokyo International Conference on Africa Development” (TICAD 7) , ambapo aliambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na viongozi wengine wa Serikali na taasisi za Umma.