Majaliwa awasimamisha vigogo wizara ya fedha kupisha uchunguzi wa mamilioni
Ameiagiza Takukuru kufanya uchunguzi huo na endapo hawatokuwa na hatia, warejee katika majukumu yao.
- Ni baada ya kubaini malipo ya fedha za umma kiholela.
- Amesema uchunguzi ukibaini kuwa hawana hatia, watarejea kazini.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi baadhi ya watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya mamilioni ya fedha za umma.
Miongoni mwa waliosimamishwa kazi na kiongozi huyo ni mkaguzi mkuu, mkaguzi msaidizi pamoja na watendaji wengine wa wizara hiyo muhimu katika kusimamia fedha za umma nchini.
Katika kikao kazi na Waziri wa Fedha na Mipango na watendaji wengine wa serikali jijini Dodoma jana (Mei 27, 2021), Majaliwa alimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) Salum Hamdun kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma hizo na ikithibitika kwamba tuhuma si za kweli wahusika watarejeshwa kazini.
Majaliwa alizitaja baadhi ya tuhuma hizo kuwa ni malipo yaliyofanyika Machi 31, Mwaka huu kupitia vocha 30 ya Sh251 milioni yakielezwa kuwa ni malipo maalum bila kutaja kazi hiyo maalum ni kazi gani na nani aliifanya hiyo kazi.
Amesema siku hiyo hiyo pia zililipwa Sh198.8 milioni kwa madai kuwa ni posho ya honoraria.
Taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu inaeleza kuwa Majaliwa amesema Aprili 8 mwaka huu watumishi 27 wa wizara hiyo walilipwa Sh44.5 milioni zikiwa ni posho ya kazi maalum ya wiki nne.
Pia, Aprili 13 mwaka huu zililipwa Sh155.2 milioni kwa watumishi 68 ikiwa ni posho ya kazi maalum ya wiki tatu.
Soma zaidi:
- Majaliwa aagiza ujenzi machinjio ya vingunguti kukamilika Juni
- Serikali kutatua migogoro ya ardhi inayomilikiwa na madhehebu ya dini
- Tanzania yashauriwa kutafakari upya kurejea mahakama ya Afrika
Aidha, Aprili 30 mwaka huu zililipwa Sh43.9 milioni kwa ajili ya kuandaa mpango wa kuhifadhi mazingira na siku hiyo hiyo zililipwa Sh14.4 milioni kwa ajili ya siku ya wanawake.
Fedha nyingine Sh43 milioni zililipwa siku hiyo na kufanya jumla ya malipo yaliyolipwa siku hiyo kuwa Sh101.8 milioni.
Majaliwa pia amesema, Mei 1 asubuhi mwaka huu zililipwa Sh184.1 milioni na mchana zililipwa Sh264 milioni zikiwa ni malipo ya kazi maalum.
“Sisi tulikuwa Mwanza tunasherehekea siku ya wafanyakazi duniani nyinyi hapa ndani mnalipana posho,” amesema Majaliwa.
Aliongeza kuwa Mei 3 mwaka huu zililipwa Sh146.5 milioni kwa watumishi 125 zikiwa ni malipo ya kuandaa Mpango Kazi wa Manunuzi, kazi ambayo ni sehemu ya majukumu yao ya jila siku. Tarehe hiyo hiyo zililipwa Sh171.2 milioni kwa ajili ya kuandaa nyaraka za Bunge.
Majaliwa amesema pesa nyingine Sh155 milioni zililipwa kwa baadhi ya watumishi zikiwa ni posho ya kuandaa muongozo wa kazi.
” Yaani hii kazi ya ukaguzi imelipwa kwenye maeneo manne, huu ni utaratibu wa wa wapi? Mnazidi kutupunguzia imani, na sijaongelea eneo la kuhamisha mafungu na utaratibu wa kuhamisha fedha kisha mnakwenda kuzichukuwa huko mlikozihamishia,” amesema Majaliwa.
Amewataka watendaji wa wizara hiyo kujenga uaminifu kwa wanaokusanya mapato kwa kufanya kazi kwa uaminifu na alitahadharisha kuwa watakaoendelea kucheza na pesa za umma hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Nimesema hapa si wote wenzenu, wachache wanatumia vibaya nafasi zao kutuchafua wizara ya fedha,” amesisitiza Majaliwa.