October 7, 2024

Majaliwa awataka Watanzania kuchangamkia fursa za masoko wiki ya viwanda

Amewata kuchangamkia fursa zitokanazo na maonyesho ya Wiki ya Viwanda ya SADC ikiwemo soko la bidhaa mbalimbali wanazotengeneza.

  • Amewata kuchangamkia fursa zitokanazo na maonyesho ya Wiki ya Viwanda ya SADC ikiwemo soko la bidhaa mbalimbali wanazotengeneza. 
  • Awataka pia kuutangaza utalii na kuvutia wageni kwenda kwenye mbuga za wanyama

Dar Es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kutumia vizuri fursa za maonyesho ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwemo kujipatia masoko ya bidhaa wanazotengeneza katika viwanda vya ndani. 

Majaliwa aliyekua akizungumza katika maonyesho hayo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa  cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, amesema maonyesho hayo yanawaleta pamoja wafabiashara wa aina zote ili wanachangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa. 

“Sisi kama Serikali tumetoa fursa kwa wale ambao wanafanya kazi na kuzalisha bidhaa zao kwa kutumia mikono kuja kuonyesha bidhaa zao ili ziweze kupata masoko kwa nchi wanachama wa SADC kwani nchi zote zinakuja hapa kuleta bidhaa mbalimbali kwa hiyo Watanzania wanatakiwa kutumia fursa hii kuwauzia wageni bidhaa zetu”, amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amesisitiza kujenga umoja kati ya wafanyabiashara waliopo nchini pamoja na wageni ili kuimarisha uzalishaji wa bidhaa zitakazokidhi soko la nchi wanachama wa SADC.


Soma zaidi: 


Sekta ya utalii nayo imetakiwa kuyatumia maonyesho hayo kujitangaza na kuvutia wageni mbalimbali kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana katika maeneo mbalimbali nchini. 

“Watanzania tutumie pia fursa ya mkutano huu wa SADC kutangaza vivutio vilivyoko nchini ili tuweze kuleta watalii kuja kutalii hapa kwetu, banda la Wizara ya Maliasili na Utalii lipo, lakini kila Mtanzania popote alipo, kwa wakati wake, atumie muda wake kuwaeleza wageni ikiwezekana kuwapeleka kwenye maeneo ya utalii kwenda kutalii.

“Aeleze kuhusu mbuga zetu kama vile Serengeti, Ngorongoro, Ruaha na Gombe, lakini pia Mlima kimanjaro, bonde la Olduvai Gorge  na fukwe zetu nzuri ili wageni waweze kutembelea maeneo haya”, amesema Majaliwa. 

Maonyesho hayo ambayo yalifunguliwa juzi na Rais John Magufuli, yanafanyika katika maeneo matatu ambayo ni ukumbi wa mikutano wa JNICC, viwanja wa Gymkhana na viwanja vya Karimjee.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama picha yake iliyochorwa kwa kutumia shanga na Aman Greon (kulia) wakati alipotembelea  Maonyesho ya Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Viwanda kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika  Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Agosti 6, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.