September 29, 2024

Majaliwa azungumzia usafirishaji makinikia nje ya nchi

Licha ya Serikali kuruhusu usafirishaji wa makinikia (mchanga wa madini), imesema makinikia yote yanayosafirishwa nje ya nchi yamefuata utaratibu na hakuna yanayouzwa bila kulipiwa kwanza.

  • Amesema kwa sasa makinikia yanaruhusiwa kusafirishwa nje ya nchi.
  • Amesema Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kusimamia mapato ya makinikia.
  • Serikali yabaini makinikia hayo yana aina tano za madini.

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kuruhusu usafirishaji wa makinikia (mchanga wa madini), imesema makinikia yote yanayosafirishwa nje ya nchi yamefuata utaratibu na hakuna yanayouzwa bila kulipiwa kwanza.

Usafirishaji wa makontena ya makinikia ulirejea Mei 2020 baada ya kukwama bandarini kwa muda mrefu kutokana kumalizwa kwa mgogoro wa kibiashara uliokuwepo kati ya kampuni ya madini ya Barrick Gold na Serikali ya Tanzania.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kwa sasa kuna usimamizi mzuri wa usafirishaji wa makinikia hayo ili kuiwezesha Serikali kupata mapato yake hata kabla mzigo haujasafirishwa. 

“Makontena yote yanayosafirishwa hivi sasa, tayari yameshauzwa na kulipiwa na fedha iko kwenye akaunti zetu. Hapo yako chini ya mnunuzi na yeye yuko huru kuyapeleka anakotaka. 

“Kwa hiyo, Watanzania hatupati hasara. Nataka niwaondolee hofu ya awali… makontena hayo yameshauzwa tayari na hakuna kontena linatoka bila kulipiwa,” amesema Majaliwa leo (Juni 3, 2020) Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Msalala, Iddi Kassim Idd kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Mbunge huyo alitaka kujua Serikali inatoa kauli gani juu ya makontena yaliyoshuhudiwa yakisafirishwa kupitia barabara ya Bulyanhulu-Kahama na bandari ya Dar es Salaam licha ya kuwa ilishazuia makinikia kusafirishwa nje ya nchi.


Zinazohusiana:


Waziri Mkuu alikiri kuwa Serikali ilishazuia usafirishaji wa makinikia kwenda nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 2017/2018 na kwamba zaidi ya makontena 300 yalizuiwa bandarini kwa sababu wahusika hawakufuata utaratibu na kulikuwa na udanganyifu.

“Makontena hayo yalizuiwa hadi tulipoweka utaratibu mpya, na utaratibu uliowekwa na Serikali ulikuwa kwanza ni kuwatambua nani asafirishe makinikia kwenda nje na nani ametoa vibali hivyo vya kwenda nje,” amesema Waziri Mkuu.

Kwa sasa, imeundwa kampuni ya madini ya Twiga ambayo Serikali ina hisa na imeingia ubia na migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara iliyo chini ya Barrick ili kuhakikisha usafirishaji huo unafanyika vizuri. 

Kuundwa kwa kampuni hiyo, Majaliwa amesema kumesaidia Serikali kubaini kuwa kuna aina tano za madini kwenye mchanga unaouzwa na siyo moja ambayo ilikuwa inatambulika awali ya dhahabu.