October 6, 2024

Majaliwa kuwasaka wadaiwa sugu nyumba za NHC

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) uwaandikie barua wapangaji wote wanaodaiwa kodi na shirika hilo zikiwemo taasisi za Serikali na wahakikishe zimelipwa ifikapo Mei 30, mwaka huu kabla

  • Wapangaji hao zikiwemo taasisi za Serikali wanadaiwa kiasi cha Sh5.6 milioni.
  • Amesema wanatakiwa kulipa kabla ya Mei 3o la sivyo atawasaka mwenyewe.
  • Aitaka NHC kukusanya kodi kielektroniki.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) uwaandikie barua wapangaji wote wanaodaiwa kodi na shirika hilo zikiwemo taasisi za Serikali na wahakikishe zimelipwa ifikapo Mei 30, mwaka huu kabla hajachukua hatua stahiki. 

Waziri Mkuu amesema madeni ambayo taasisi za Serikali zinadaiwa pekee yanafikia Sh4.3 bilioni na kama zitalipwa zote hizo, zitalisaidia shirika kuendelea na mpango wake wa ujenzi wa nyumba nafuu kwenye maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

 “Orodha ya wadaiwa niliyonayo hapa ni kubwa na wengine inaonyesha wamehama na wameondoka bila kumalizia kodi zao. Hawa wote ni lazima tuwafuatilie na walipe madeni yao,” amesema leo (Februari 11, 2020)  wakati akizungumza na viongozi na wajumbe wa Bodi ya shirika hilo kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwake, Magogoni, jijini Dar es Salaam.

 Amesema taasisi zote za Serikali ambazo zimepanga kwenye nyumba za shirika ni lazima zilipe madeni kwa sababu chombo chochote cha Serikali kinaishi na bajeti, kwa hiyo hata kama wamejenga ya kwao, walipaswa walipe kabla hawajahama.

 “Waandikieni barua wadaiwa wote ili walipe. Tunaelekea mwishoni mwa bajeti ya mwaka huu, na hawa wote wawe wamelipa ifikapo tarehe 30 Mei, 2020. Nami nipate orodha ya taasisi za Serikali zinazodaiwa ili niwafuatilie; nitawaita Makatibu Wakuu wao mmoja mmoja. Hao wadaiwa binafsi wachukulieni hatua stahiki,” amesisitiza.


Soma zaidi: 


Wakati huohuo, Waziri Mkuu amelitaka shirika hilo lijielekeze kwenye ujenzi wa nyumba bora na za bei nafuu kwa sababu mahitaji ya nyumba nchini bado ni makubwa. 

“Simamieni suala hili, ili tupate nyumba nzuri na za bei nafuu. Simamieni wataalamu wenu ili wasikadirie miradi ambayo bei zake zitakuwa juu sana na kisha wananchi wetu washindwe kumudu. Ni lazima mhakikishe kuwa wananchi wa kipato cha chini wananufaika na uwepo wa shirika,” amesema.

 Amesema wataalamu hao wanahitaji kudhibitiwa kwa sababu sehemu kubwa ya malighafi inapatikana hapa nchini zikiwemo kokoto, nondo, mabati na vifaa vingi vya ujenzi vinazalishwa hapa nchini.

 Pia Majaliwa amewataka viongozi hao waimarishe ukusanyaji wa mapato ya shirika hilo kwa kuhakikisha kodi zinakusanywa kwa njia ya kielektroniki. 

 “Tuache tabia ya kuruhusu maafisa kwenda nyumba kwa nyumba na kudai shilingi 500,000 kwa risiti za kuandika. Tumieni control number, ili mwananchi aweze kulipia kwa simu au benki na hela inaingia moja kwa moja katika shirika,” amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa  (NHC), ofisini kwake Magogoni jijini Dar es salaam, Februari 11, 2020. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mapema, akitoa taarifa ya shirika hilo mbele ya Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Sophia Kongele amesema shirika hilo linawadai wapangaji waliohama na waliopo ambao wengi wao ni wizara na taasisi za Serikali na akaomba wahimizwe kulipa ili wao waweze kuendesha shirika kwa ufanisi.

 “Kwa wapangaji waliohama bila kulipa, shirika linadai Sh4.353 bilioni na kwa wapangaji waliopo wanadaiwa kiasi cha Sh1.286 bilioni na hivyo kufanya deni lote lifikie shilingi bilioni 5.641.”

 Amesema shirika hilo limekuwa likiendesha miradi ya ndani na ya nje ikiwemo kutekeleza miradi ya ujenzi ya taasisi nyingine kama mkandarasi na mshauri.

 Amesema wanaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mikubwa ya Morocco Square, Seven Eleven (Kawe), Golden Premier Residence (Kawe) na Regent Estate ambayo kwa sasa imesimama kutokana na ukosefu wa fedha.