July 5, 2024

Majiko banifu yatakavyopunguza ukataji wa miti Tanzania

Majiko hayo ambayo hutengenezwa kwa malighafi za vyuma na mapati yanatumia kuni mbili tu, jambo linalosaidia kupunguza ukataji wa miti.

  • Ni njia rahisi ya kupunguza ukataji wa miti na matumizi ya mkaa na kuni.
  • Wadau wa mazingira washauri nishati endelevu ikiwemo matumizi ya gesi na umemejua kumaliza tatizo hilo.
  • Serikali yasema itaendelea kushirikiana na wadau kutafuta suluhu ya kudumu ya ukataji wa miti. 

Dar es Salaam. Huenda ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa ukapungua katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani baada ya teknolojia ya majiko banifu yanayotumia kuni chache kuingia wilayani humo. 

Licha ya kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo sehemu kubwa ya ardhi yake imezungukwa na miti, iko katika hatari ya kutoweka, ikiwa suluhu za nishati safi na endelevu hazitapewa kipaumbele ili kuwasaidia wananchi hasa wa vijijini kuachana na matumizi ya mkaa na kuni.

Mwongozo wa upandaji na utunzaji wa miti Tanzania uliotolewa na Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA) uliotolewa mwaka 2017, unaeleza kuwa misitu imefunika hekta zaidi ya milioni 48 ya ardhi ya Tanzania.

Eneo hilo la misitu ni zaidi ya jimbo moja la California nchini Marekani.

Lakini ukataji wa miti usiodhibitiwa kwa ajili ya mkaa na kuni zinazotumiwa nyumbani na viwandani unatishia uwepo wa misitu hiyo ambayo ina umuhimu katika kuendelea mifumo ya maisha ya wanyama na mimea, kupunguza mmonyoko wa udongo na uzalishaji wa hewa ukaa na kutunza vyanzo vya maji.  

Kwa mujibu wa Ripoti ya Taifa ya Takwimu za Mazingira ya mwaka 2017 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kiwango cha ukataji miti kinakadiriwa kuwa ni hekta 372,000 kwa mwaka.

Kutokana na changamoto hizo za ukataji wa miti ambazo zinachangia mabadiliko ya tabianchi, baadhi ya wadau wa mazingira wanaendelea na jitihada za kutafuta suluhu endelevu za kupunguza tatizo hilo nchini Tanzania. 

Baadhi ya wakazi wa vijiji vya Kidomile na Makurunge katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wameanza kuachana na matumizi ya mkaa na kuni na kugeukia matumizi ya majiko banifu (budget firewood cooking stoves) kwa ajili ya kupikia.

“Nina jiko banifu ambalo nimetengeneza mwenyewe linalotumia kuni chache kupika vyakula vingi kwa wakati mmoja, jambo ambalo ni tofauti na zamani ambapo matumizi ya kuni yalikuwa makubwa nyumbani,” anasema Ramadhan Rajab, mkazi wa kijiji cha Kidomile aliyenufaika na mafunzo ya teknolojia ya utengenezaji wa majiko hayo kutoka taasisi ya CAN Tanzania. 

Ramadhani akiangalia jiko banifu linavyofanya kazi baada ya kukamilisha kulitengeneza wakati wa mafunzo yaliyotolewa na CAN Tanzania. Picha| CAN Tanzania.

Majiko hayo ambayo hutengenezwa kwa malighafi za vyuma na mapati yanatumia kuni mbili tu kwa wakati mmoja kupikia, jambo linaloondoa usumbufu wa wanawake kutumia muda mwingi kutafuta nishati porini ili kukidhi mahitaji ya familia.

“Kwa sasa nakusanya kuni chache angalau mara moja kwa wiki,” anasema Marium Aziz, mkazi wa kijiji cha Makurunge kuhusu ufanisi wa majiko hayo. 

“Ninaweza kukaa na watoto wangu jikoni kwa sababu jiko hilo linatoa moshi mchache. Wakati tunatumia majiko ya udongo ya mafiga matatu, moshi ulikuwa mwingi na kuwasababishia watoto kukohoa mara kwa mara na macho kuwa mekundu,” anasema Marium.

Majiko hayo ambayo yanadumu muda mrefu yanatoa moshi mchache, yanalinda na kuboresha afya ya familia; na wanawake kama Marium wanaweza kupata muda wa kukaa na familia na kufanya shughuli za ujasiriamali ili kujipatia kipato.

Huenda matumizi ya majiko hayo yatasaidia kupunguza shughuli za ukataji wa miti katika Wilaya ya Bagamoyo endapo wadau wa mazingira watayapa msukumo wa kipekee ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Lakini wapo wanaotumia majiko hayo yaliyotengenezwa kwa udongo mfinyanzi ili kuepuka gharama za kununua majiko banifu yaliyotengenezwa kwa vyuma ili kurahisisha maisha.

Licha ya umuhimu wake katika kuboresha maisha na utunzaji wa mazingira bado watu wengi hawatumii majiko hayo kwa sababu ya ukosefu wa elimu na gharama za majiko hayo ambazo wananchi wa kawaida hawawezi kumudu.


Soma zaidi: 


Msimamizi wa miradi kutoka CAN Tanzania, Jophillene anasema waliamua kutoa mafunzo ya utengenezaji wa majiko hayo baada ya kubaini kuwa asilimia 42 za kaya katika Wilaya ya Bagamoyo hazifahamu umuhimu wa nishati safi ya kupikia huku asilimia 91 ya kaya hizo zikitegemea mkaa na kuni kama nishati ya msingi ya kupikia. 

“Haya mafunzo ni miongoni mwa jitihada za kuhamasisha wananchi wa Bagamoyo kuachana na kuni na kugeukia mifumo ya nishati safi na rahisi ya kupikia,” anasema Bejumula.

Bejumula anasisitiza kuwa majiko hayo yawe chachu kwa Serikali na wadau wa mazingira kuongeza kasi ya kuwawezesha wananchi kutumia nishati jadidifu ikiwemo umemejua ambazo zinatoa suluhu endelevu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. 


Majiko banifu ni njia endelevu ya kuzuia ukataji wa miti?

Kazi ya majiko banifu ni kupunguza ukataji wa miti kwa kuwawezesha wananchi kutumia kuni chache wakati wa kupika na siyo njia ya kudumu itakayoweza kumaliza tatizo la ukataji miti nchini. 

Repoti ya ufuatiliaji wa matumizi ya majiko banifu yaliyoboreshwa ya mwaka 2013 iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Chama Cha Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA) inaeleza kuwa majiko banifu hasa ya chuma ni maboresho yaliyofanyika kwenye majiko ya asili ambayo hutengenezwa kwa udongo.

Ili kuyaongeze ufanisi, ripoti hiyo inapendekeza kuwa itumike nishati nyingine ikiwemo mabaki ya mimea na wanyama kuliko kuni au mkaa ili kuhakikisha miti haikatwi kwa ajili ya shughuli za kupikia. 

“Teknolojia mpya za kupikia ikiwemo za majiko ya gesi ambayo yanatumia nishati ya mabaki ya mimea iwekewe mkazo kwenye jamii,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wa nishati safi na endelevu wanapendekeza matumizi ya nishati jadidifu ambazo zimeonyesha matukio mazuri katika kutunza miti ya asili na ile ya kupandwa. 

Mtaalam wa masuala ya nishati jadidifu kutoka Mtandao wa Jinsia na Nishati Endelevu Tanzania (Tangsen), Thabit Mikidadi anasema kuna umuhimu wa kuangazia teknolojia zinazotumia nishati ndogo ya umeme na gesi ambazo hupunguza au kuondoa kabisa hitaji la kutumia mkaa na kuni. 

“Pia gesi ni nishati nzuri ambayo watu wa kipato cha juu na cha kati wanaweza kuitumia hasa mijini kwa kuwa upatikanaji wake umerahisishwa na bei yake si kubwa sana. Pia nishati mbadala kama mkaa mbadala (briquettes) ni njia nzuri katika kutunza mazingira,” anasema Mikidadi.

Ili kupiga hatua ya kuwa na mifumo endelevu ya kupikia, Mikidadi anashauri Serikali na wadau wa nishati kuweka mipango inayotekelezeka, kuongeza ufadhili wa kifedha na kufanya utafiti wa tabia na tamaduni za watu kuhusu matumizi ya nishati ya kupikia. 

Waziri wa Muungano na Mazingira, Mussa Azzan Zungu katika hutuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2020/21 anasema wataendelea kushirikiana na wadau wa nishati kutoa elimu na kuhimiza matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza matumizi ya mkaa na kuni. 

“Wizara itaendelea kuhamasisha jamii kuhusu matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yana athari kubwa kwenye mazingira,” anasema Zungu.