November 24, 2024

Majina waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano 2020 bayana

Mwanafunzi bora kidato cha nne 2019 apelekwa Kilakala mkoani Morogoro.

  • Wanafunzi 121,251 wamechaguliwa kujiunga na ngazi hizo za elimu wakiwemo wasichana 53,829.
  •  Katika majina hayo mapya, aliyekuwa mwanafunzi bora kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne, Joan Ritte amechaguliwa kujiunga na shule ya vipaji maalum ya Kilakala iliyopo mkoani Morogoro.

Dar es Salaam. Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imetoa orodha ya majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano, vyuo vya ufundi na ualimu kwa mwaka 2020 ikiwa ni dakika chache baada ya Serikali kutangaza utaratibu wa kurejea shuleni kwa wanafunzi waliokuwa wamefunga shule kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona. 

Waziri wa Ofisi ya Rais-Tamisemi Suleiman Jafo amewaambia wanahabari Jumatano (Juni 17, 2020) kuwa wanafunzi 121,251 wamechaguliwa kujiunga na ngazi hizo za elimu wakiwemo wasichana 53,829. 

Wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na shule za bweni wanatakiwa kuripoti shuleni Julai 18, 2020 ili kuanza masomo Julai 20, Jafo amesema. 

Wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana walikuwa wakisubiri kwa hamu taarifa hizo ambazo ni muhimu katika safari yao ya kupata elimu ya juu nchini. 


Zinazohusiana:


Katika majina hayo mapya, aliyekuwa mwanafunzi bora kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne, Joan Ritte amechaguliwa kujiunga na shule ya vipaji maalum ya Kilakala iliyopo mkoani Morogoro.

Ritte amechaguliwa kusoma mchepuo wa PCM ukihusisha Fizikia, Kemia na Hisabati. 

Mbali na kuwachagua wanafunzi kwenda kidato cha tano, Tamisemi imewachagua wanafunzi kwenda kusoma astashahada mbalimbali katika vyuo vya umma ikiwemo stashahada ya awali ya ualimu.

Majina hayo yametangazwa dakika chache baada ya wizara ya elimu, sayansi na teknolojia kutangaza utaratibu wa kurejea kwa masomo kwa wanafunzi wote waliokuwa wamefunga shule kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona ikiwemo shule za msingi na awali.

Kufahamu mwanafunzi amechaguliwa kwenda shule au chuo gani bonyeza hapa