October 6, 2024

Makamba atoa ufafanuzi wa matumizi ya mifuko ya plastiki kwenye ndege

Amesema mpaka sasa wageni wanaoingia nchini hawajazuiwa kutumia mifuko hiyo na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) itatoa utaratibu wa matumizi ya mifuko hiyo kwenye ndege.

Amesema hakuna mtalii atakayeingia nchini akiwa na mifuko ya plastiki atakayekamatwa lakini watakaokuja nayo wataelekezwa kuikabidhi kwa mamlaka husika na kushauriwa kupata mifuko mbadala. Picha|Mtandao.


  • Amesema mpaka sasa wageni wanaoingia nchini hawajazuiwa kutumia mifuko hiyo.
  • Amesema Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) itatoa taarifa rasmi ya matumizi ya mifuko hiyo kwenye ndege.
  • Serikali imesema haitawakamata watalii bali wataelimishwa kutumia mifuko mbadala. 

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano na Mazingira), January Makamba amesema Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) itatoa taarifa rasmi kuhusu matumizi ya mifuko ya plastiki kwenye ndege zinawaleta wageni nchini na hakuna mtalii atakayekamatwa kwa matumizi ya mifuko hiyo. 

Kauli ya Makamba inakuja baada ya kusambaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii kuwa wageni wote wanaokuja nchini hawaruhusiwi kuwa na mifuko ya plastiki na watakaofanya hivyo wataadhibiwa. 

Ametoa ufafanuzi huo katika ukurasa wake wa twitter ambapo amesema taarifa hizo siyo za kweli na zinapotosha kwa sababu mpaka sasa Serikali haijazuia matumizi ya mifuko ya plastiki yenye zipu inayotumiwa na wasafiri wa kimataifa. 

“Haya mabandiko yanapotosha. Mamlaka ya Viwanja vya Ndege  itatoa taarifa rasmi kwa wasafiri wa kimataifa wanaotumia mashirika ya ndege. Kwa kuanzia, mifuko yenye zipu haijazuiwa,” inasomeka sehemu ya ujumbe wa Makamba katika mtandao wa Twitter. 

Amesema hakuna mtalii atakayeingia nchini akiwa na mifuko ya plastiki atakayekamatwa lakini watakaokuja nayo wataelekezwa kuikabidhi kwa mamlaka husika na kushauriwa kupata mifuko mbadala.

Aprili 9, 2019 Waziri mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza rasmi marufuku ya matumizi ya mifuko ya  plastiki nchini ifikapo Juni 1 mwaka huu ambapo marufuku hiyo itahusisha utengenezaji, ununuzi na kuuza ili kunusuru uharibifu wa mazingira, vifo kwa wanyama na kuziba kwa mitaro.


Zinazohusiana:


Wadau wanaohusika na mifuko hiyo wametakiwa kujielekeza katika kuanzisha viwanda vya kutengeneza mifuko mbadala ikiwemo mifuko ya karatasi.

Hata hivyo, marufuku hiyo haitahusu mifuko inayotumika kukusanyia taka katika ndoo za takataka (trash bags) inayotumika kama vifungashio vya bidhaa mbalimbali ikiwemo za kilimo.