October 7, 2024

Maktaba ya mtandaoni inayosaidia kupata habari za Corona

Inajumuisha habari na matangazo mbalimbali yanayowekwa na watumiaji wa mtandao huo.

  • Ni maktaba ya “Ad Library” ya mtandao wa Facebook.
  • Inajumuisha habari na matangazo mbalimbali yanayowekwa na watumiaji wa mtandao huo.
  • Pia inatumika kuthibitisha matangazo halali ya Corona ili kuepuka uzushi.

Dar es Salaam. Mitandao ya kijamii, imekuwa ni njia mojawapo inayotumiwa kupenyeza habari za uzushi hasa wakati huu ambao dunia inapambana kutokomeza janga la Corona (COVID-19).

Hata hivyo, mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook imejidhatiti kuhakikisha inawalinda watumiaji wake dhidi ya athari za habari za uzushi zinazolenga kuwapotosha watu kuhusu COVID-19.

Facebook imeanzisha programu mbalimbali za kidijitali ili kupambana na uongo wa kila aina kwenye mtandao huo unaokua kwa kasi.

Tayari imefuta na hairuhusu matangazo yanayohusu matibabu ya COVID-19 na imeanzisha maktaba maalum ya matangazo inayojulikana kama “Ad Library” ambayo ina matangazo yote yanayowekwa na watumiaji wake.

“Ad Library” inasaidia kufahamu watu wanaotangaza bidhaa au huduma kupitia Facebook na watu waliofikiwa ikiwemo yale yanayohusu Corona.

Kwa watu ambao wanapokea matangazo kutoka Facebook hasa ya ugonjwa huo, wanaweza kuitumia programu hiyo kuthibitisha kama ni ya kweli au yanapotosha, licha ya kuwa mtandao huo umezuia matangazo ya Corona.


Zinazohusiana:


Unawezaje kuitumia?

Ili kuitumia programu hiyo, unatakiwa kufungua Facebook na kwenda kwenye kipengele cha “Page Transparency” ambacho kitakuwezesha kuingia mpaka sehemu ya Ad Library ambapo utakutana na matangazo mbalimbali ya mtandao huo.  

Pia unaweza kuingia katika maktaba hiyo ya Facebook kwa  kupitia  kitafutio cha mtandao wa Google kwa kutafuta  neno Ad Library na kukupeleka moja kwa moja hadi kwenye ukurasa huo.

Ukifika kwenye ukurasa huo utaweza kwenda kwenye sehemu ya kutafuta ‘search’ na kuweka tangazo ambalo analitilia mashaka kisha ataweza kupata taarifa zake moja kwa moja kwa ndani zaidi.

Kumbuka mapambano dhidi ya Corona yanamuhusi kila mtu, timiza wajibu wako kwa kuthibitisha kila habari au tangazo unalopokea kabla ya kusambaza kwa wengine.