July 8, 2024

Malipo deni la Serikali kutawala bajeti wizara ya fedha ya 2020-2021

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango amesema katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 inakadiria kutumia bajeti ya Sh12.39 trilioni huku zaidi ya robo tatu ya fedha hizo zitatumika kulipa deni la Taifa.

  • Asimilia 84.5 ya bajeti yote ya wizara hiyo itatumika kulipa deni la Serikali.
  • Bajeti ya 2020/2021 imeongezeka hadi Sh12.39 trilioni kutoka Sh11.94 trilioni ya mwaka 2019/2020. 

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango amesema katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 inakadiria kutumia bajeti ya Sh12.39 trilioni huku zaidi ya robo tatu ya fedha hizo zitatumika kulipa deni la Serikali. 

Bajeti ya wizara hiyo ndiyo bajeti ya kiwango cha juu kuliko bajeti zote zilizowasilishwa katika Bunge la bajeti la mwaka huu. 

Dk Mpango katika hotuba yake ya bajeti iliyowasilishwa leo (Mei 15, 2020) Bungeni jijini Dodoma amesema bajeti hiyo itagawanywa katika mafungu saba kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo. 

“Kati ya kiasi hicho, Sh11.73 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh659 bilioni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo,” amesema Dk Mpango. 

Waziri huyo amesema kati ya fedha za matumizi ya kawaida, Sh10.48 trilioni ni kwa ajili ya deni la Serikali na fedha zilizobaki zitaelekezwa katika matumizi mengineyo, mishahara na maendeleo.Hiyo ni sawa na kusema asilimia 84.5 ya bajeti yote ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa 2020/2021 itaelekezwa kulipa deni la Serikali.


Soma zaidi:


Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha na Mipango hadi kufikia Novemba 30, 2019 deni la Serikali lilikuwa Sh54.84 trilioni, kati ya fedha hizo Sh40.39 trilioni ni deni la nje.  Hata hivyo, Dk Mpango amesema hadi kufikia Machi 2020, Serikali ilifanikiwa kulipa deni lake lote lililoiva lenye thamani ya Sh6.19 trilioni.

Amesema kwa mwaka 2020/21, wizara itaandaa na kutekeleza mikakati itakayowezesha Serikali kukopa katika soko la fedha la ndani na nje bila kuathiri uhimilivu wa deni la Serikali, Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada Sura 134 na vigezo vya viashiria hatarishi vya madeni yaliyotokana na dhamana za Serikali.

Bajeti ya mwaka ujao wa 2020/2021 imeongezeka kwa Sh45 bilioni kutoka Sh11.94 trilioni ya mwaka huu unaoisha mwezi Juni.

Kwa mujibu wa Dk Mipango hadi Machi 2020, wizara yake imetumia jumla ya Sh7.69 trilioni sawa na asilimia 64.40 ya bajeti iliyoidhinishwa mwaka 2019/2020.