October 6, 2024

Malipo ya wakulima wa korosho yafikia Sh500 bilioni

Fedha hizo ni kati ya Sh700 bilioni zinazotarajiwa kulipwa kwa wakulima hao kabla ya zoezi hilo kuhitimishwa Februari 15, 2019.

Korosho ni zao la biashara linaloongoza kuingiza fedha za kigeni nchini. Picha|Mtandao.


  • Fedha hizo ni kati ya Sh700 bilioni zinazotarajiwa kulipwa kwa wakulima hao kabla ya zoezi hilo kuhitimishwa Februari 15, 2019.
  •  Serikali imesisitiza kununua korosho daraja la kwanza kwa bei ya Sh3,300  nadaraja la pili  kwa Sh2,600 ambazo ni asilimia 80 ya zile za daraja la kwanza.

Dar es Salaam. Ikiwa zimepita zaidi ya wiki tatu tangu Serikali kuitaka Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) kubadili mfumo wake ili kuharakisha malipo kwa wakulima wa korosho, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema zaidi ya Sh500 bilioni zimelipwa kwa wakulima hao kati ya Sh700bilioni zinazotarajiwa kulipwa.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa tamko la Rais John Magufuli la kuwa Serikali itanunua korosho kwa bei ya Sh3,300 ni kwa ajili ya korosho za daraja la kwanza  na bei ya korosho za daraja la pili ni asilimia 80 ya zile za daraja la kwanza.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo (Februari 7, 2019) Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka.

 Mbunge huyo alitaka kujuakauli ya Serikali kuhusu malipo kwa wakulima wa korosho ambao walikuwa wakilipwa Sh2,600 kwa kilo wakati Rais Magufuli alisema Serikali itanunua kilo moja ya korosho kwa Sh3,300.

“Malipo yanaendelea na sehemu kubwa ni kwa wakulima wenye kilo zaidi ya 1,500, Serikali itanunua korosho zote kama ilivyoelezwa. Taratibu zinazofanyika ni kuhakikisha anayelipwa ni muhusika. Wananchi endeleeni kuiamini Serikali yenu,” amesema Majaliwa.


Zinazohusiana:


 Amesema ilikuwa ni lazima kwa Serikali ifanye uhakiki kwa wakulima hususani wale wenye kilo zaidi ya 1,500 ili kujiridhisha kama ni wakulima, hivyo baada ya kuhakikiwa wakulima wote watalipwa fedha zao.

 Serikali inatazamia kuwa hadi kufikia Februari 15 mwaka huu, Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko watakuwa wamekamilisha zoezi la uhakiki na kuwalipa wakulima wa korosho.

Zoezi la uhakiki na malipo lilianza Novemba 27, 2018 na lilitakiwa kukamilika Januari 10 mwaka huu lakini changamoto mbalimbali ikiwemo kutofatiana kwa  taarifa za kibenki zilizowasilishwa na majina ya wakulima waliouza mzigo wa korosho.  

Januari 27, 2019 Majaliwa alifanya mazungumza na wadau wa zao hilokwenye kikao kilichofanyika mkoani Mtwara ilikupata taarifa juu ya mwenendo mzima wa uzalishaji wa korosho kwa msimu wa mwaka 2018/2019 ili kuepusha matatizo yaliyojitokeza katika msimu uliopita.