Mama Samia ahimiza matumizi mifumo ya kidijitali sekta ya afya
Amesema mifumo hiyo itasaidia kuondoa pengo la utoaji wa huduma za afya na kusaidia katika ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika Mashariki.
- Amesema mifumo hiyo itasaidia kuondoa pengo la utoaji wa huduma za afya na kusaidia katika ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika Mashariki.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwekeza katika mifumo ya kidijitali na teknolojia katika sekta ya afya ili kupata mafanikio ya kweli na endelevu ya ukuaji wa uchumi katika nchi zao.
Amesema uwekezaji huo utasaidia katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) ifikapo 2030 hasa lengo la tatu linalosisitiza afya bora kwa watu wote.
Mama Samia aliyekuwa akizungumza leo (Machi 27,2019) jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Afya na Sayansi la Afrika Mashariki (EAHSC) amesema uwekezaji katika sekta ya afya ni muhimu kwa maendeleo na juhudi za kuwekeza katika mifumo hiyo inahitajika sana katika jumuiya hiyo.
“Nimeridhishwa na juhudi za jumuiya za utekelezaji wa mkataba wa EAC, hasa ibara ya 118 ambayo inahimiza ushirikiano katika sekta ya afya na vipengele vingine vinavyohusiana na mkataba wa soko la pamoja la EAC,” amesema Mama Samia.
Amesema sayansi na teknolojia ni vyombo muhimu katika kutatua changamoto na pengo la huduma za afya ambazo zinahitajika kuhakikisha watu wanakuwa na afya bora kuwawezesha kutimiza shughuli za kijamii na uchumi.
Soma zaidi: Teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi wa matibabu ya figo Muhimbili
Akitolea mfano, amesema Tanzania imeanza kuchukua hatua za kuhakikisha sekta ya afya inaunganishwa katika mifumo ya kidijitali ikiwemo Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kutumia teknolojia ya kisasa kufuatilia usambazaji wa dawa; Mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya (NHIF) ina mfumo wa usimamizi wa wanachama, michango na madai yao.
“Katika mamlaka zetu tumefunga mifumo ya usimamizi wa hospitali katika hospitali zote za Serikali,” amesema Mama Samia.
Washiriki wa Kongamano la Afya na Sayansi la Afrika Mashariki (EAHSC) linalofanyika jijini Dar es Salaam wakimsikiliza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye hayuko pichani. Picha| Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kupitia mapinduzi hayo ya kidijitali katika sekta ya afya, amesema ufanisi wa utoaji huduma umeaimarika, upatikanaji wa takwimu sahihi kwa ajili ya maamuzi ya kisera na uwazi na uwajibikaji katika sekta hiyo nao umeongezeka.
Kongamano hilo linafanyika kila baada ya miaka miwili unawakusanyisha wadau wa sekta za afya kutoka Afrika Mashariki na Wataalamu kutoka sehemu mbalimbali duniani ambao una lengo la kuangalia namna ya kutumia utaalamu wa kisasa katika huduma ya afya kwa kutumia mfumo wa kidijitali.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema Kongamano hili linafanyika wakati ambapo Afrika inahitaji mabadiliko ya teknolojia ya haraka hasa katika teknolojia ya kidijitali ili kusaidia utekelezaji wa hatua za sekta za afya na mipango na kuongeza kasi ya kufikia Ufikiaji wa Afya wa Ulimwengu (UHC) ili kufikia kufikia Malengo la Maendeleo Endelevu (SDG).