October 6, 2024

Mama Samia ataka hatua zichukuliwe kukabiliana na viumbe vamizi

Asema visipodhibitiwa mapema vitageuka janga kwa uchumi wa Taifa, mazingira na afya za wananchi.

  • Asema visipodhibitiwa mapema vitageuka janga kwa uchumi wa Taifa, mazingira na afya za wananchi.
  • Wadau wa sekta za umma na binafasi kushirikiana katika mapambano dhidi ya viumbe hao.
  • Viumbe hao wanatokana na sababu mbalimbali zikiwemo shughuli za kibinadamu na maendeleo ya mfumo wa usafiri duniani.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wadau wa sekta za umma na binafasi kushirikiana katika mapambano dhidi ya viumbe vamizi ili kuliepusha Taifa kuingia gharama kubwa za kukabiliana na janga hilo hapo baadaye.

Mama Samia ametoa maagizo hayo wakati wa uzinduzi wa Kikosi Kazi cha Kutatua Changamoto za Viumbe Wageni/ Vamizi nchini uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam ambapo amesema viumbe hao bado hawajashughulikiwa vizuri na jitihada za makusudi zinahitajika kumaliza tatizo.

“Pamoja na kwamba viumbe hawa ni janga la kiuchumi, kimazingira na kiafya  lakini bado halijashughulikiwa kikamilifu hususani katika elimu ya kuzuia viumbe hawa na kuwa na mipango madhubuti ya kukabiliana nalo,” amesema.

Amezitaka sekta na taasisi zote zifanye kazi kwa pamoja kwa kupeana taarifa na mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo ushirikishwaji wa wadau wote wakiwemo, Halmashauri za wilaya ,Wizara za kisekta, Serikali za Mitaa, Asasi za Serikali na zisizo za Serikali, Sekta binafsi pamoja na wananchi pamoja na vyombo vya habari.

“Kama tulifanya makosa huko nyuma kushughulikia jambo hili kila sekta kivyake tangu sasa tuache,” amesema.  


Zinazohusiana:


Akitoa rai kwa waliochaguliwa kuunda Kikosi Kazi cha Kitaifa, Mama Samia amesema  watambue kuwa wamepewa jukumu kubwa la kulisimamia suala hilo la viumbe vamizi kikamilifu na kuwataka kufanya kazi kulingana na hadidu za rejea  ili kuleta matokeo chanya ya kazi waliyopewa na Taifa.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wadau wa sekta za umma na binafasi kushirikiana katika mapambano dhidi ya viumbe vamizi. Picha| Mtanzania.

Kikosi kazi hicho chenye wajumbe 18 kitaongozwa na Mwenyekiti wake Dk Ezekiel Mwakalukwa ambaye atakuwa na jukumu kubwa la kuwaongoza wenzake kufikia malengo yaliyowekwa.

Viongozi wengine waliohudhuria uzinduzi huo ni Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Juma Awesu, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega pamoja na wadau mbali mbali wa mazingira.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano wa Mazingira, January Makamba amesema kuwa aligundua tatizo la viumbe vamizi mara baada ya kufanya ziara katika mikoa mbalimbali nchini ambapo amekuta athari za mimea na viumbe vamizi zimekuwa kubwa na tishio kwa wananchi hivyo kuona kuna kila sababu ya kuanza kulishughulikia.

“Tishio kubwa la hifadhi ya Ngorongoro ni kuwepo kwa mimea ambayo wanyama hawawezi kula na sio tu hapo lakini hata katika hifadhi za Serengeti na Saadan hali ipo hivo pia,” amesema Makamba.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Profesa Dos Santos Silayo amesema uwepo wa viumbe hao unatokana na sababu mbalimbali zikiwemo shughuli za kibinadamu, maendeleo ya mfumo wa usafiri duniani akitolea mfano meli, mizunguko ya wanyama kutoka eneo moja na jingine na mabadiliko ya tabia nchi pia huchangia kuleta viumbe wavamizi.

Viumbe vamizi ni viumbe wasio asili katika eneo wanaloishi na ambao huongezeka idadi na kustawi pasipo udhibiti na kubadili au kuharibu ustawi wa viumbe wengine katika eneo husika. Kwa maana hiyo, aina fulani ya kiumbe anaweza akawa sio wa asili katika eneo analoishi lakini pia asiwe kiumbe vamizi, lakini viumbe vamizi wote ni viumbe wasio asili katika maeneo wanayopatikana.

Kwa mujibu wa kanzi data ya Global Invasive Species Database, Tanzania ina takribani viumbe vamizi 100. Baadhi ya viumbe ambao watu wengi tunawafahamu ni samaki aina ya sangara (Lates nilotica) katika Ziwa Victoria, Mimea aina ya magugu maji (Eichhornia crassipes), ndege aina ya kunguru (Indian house crow), mimea aina ya mishona nguo (Bidens pilosa) na viumbe wengine wengi