Mama Samia atoa salamu za Magufuli kwa Watanzania
Salamu za Rais Magufuli kupitia kwa Mama Samia zinakuja wakati kukiwa na mjadala hasa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na baadhi ya watu vikiwemo vyama vya upinzani kuhoji kuhusu afya na alipo Rais John Magufuli.
- Amesema Rais amewataka Watanzania kuchapa kazi na kujenga Taifa lao kwa sababu nchi iko salama.
- Mama Samia naye awataka Watanzania kushikamana na kujenga umoja na kuacha kusikiliza maneno ya nje.
- Mpaka sasa kuna mjadala mtandaoni kuhusu afya na alipo Rais John Magufuli ambaye hajaonekana hadharani tangu Februari 27, 2021.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuacha kusikiliza na kubabaishwa na maneno ya nje kwa sababu yanavuruga umoja wa Taifa huku akiwasilisha salamu za Rais John Magufuli kwa Watanzania kuwa “wachape kazi, nchi iko salama.”
Salamu za Rais Magufuli kupitia kwa Mama Samia zinakuja wakati kukiwa na mjadala hasa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na baadhi ya watu vikiwemo vyama vya upinzani kuhoji kuhusu afya na alipo kiongozi huyo wa juu nchini.
Mara ya mwisho Rais Magufuli alionekana hadharani Februari 27, 2021 wakati akimuapisha Katibu Mkuu Kiongozi mpya Dk Bashiru Ally Ikulu mkoani Dar es Salaam.
“Anawasilimia sana, anasema tuko salama tuchape kazi twende vizuri, tujenge upendo na mshikamano wa Watanzania ili Taifa letu likue liwe na tija zaidi,” Mama Samia amesema leo Machi15, 2021 wakati akitoa salamu za Rais Magufuli mara baada ya kuzindua kiwanda cha kuchakata mazao ya nafaka kilichopo Michungwani katika Halmashauri ya Handeni mkoani Tanga.
Akiwa njiani wakati anaelekea kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ghorofa moja la Halmashauri ya Wilaya ya Handeni vijijini linalojengwa mjini Mkata, makamu wa Rais amesisitiza kuwa nchi iko salama na Watanzania wanapaswa kushikamana kipindi hiki kuliko kipindi chochote.
“Nawaomba wote tushikamane kwa umoja, mshakamano wetu kama Watanzania…tuendelee kuchapa kazi kama sisi tulivyokuja tunachapa kazi tunaangalia miradi, watu wote shughulikeni na mambo yenu jengeni Taifa lenu,” amesema kiongozi huyo wa nchi.
Soma zaidi:
- Safari ya mwisho ya Maalim Seif kuhitimishwa leo Zanzibar
- Magufuli, Watanzania wamlilia Maalim Seif
- Majaliwa: Rais wenu yuko imara, anafanya kazi zake kama kawaida ofisini
Mama Samia, ambaye alikuwa akizungumza juu gari, amesema Watanzania hawapaswi kuyumbishwa na maneno ya mitandaoni na watu kutoka nje kuhusu Taifa la Tanzania.
“Nataka kuwahakikishia ndugu zangu Tanzania tuko salama. Ni kawaida ya mwanadamu kukaguliwa kaguliwa, leo mafua mara homa, mara hiki, chochote kile.
“Katika wakati muhimu wa Watanzania kushikamana ni wakati huu, kujenga umoja ni wakati huu. Si wakati wa kusikiliza maneno yanayotoka nje nasi yakatuparaganya vichwa,” amesisitiza Mama Samia.
Mama Samia anakuwa kiongozi wa pili wa juu kusisitiza Watanzania kushikamana na kutosikiliza mambo kutoka nje ya nchi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa mkoani Njombe Machi 12, 2021 alisisitiza kuwa Rais Magufuli yuko imara na anaendelea na majukumu yake ofisini.
“Kumzushia ugonjwa ni chuki. Niseme wewe unaumwa! Inasaidia nini? Atoke! Aende wapi? Aende nje! Afanye nini? Uliwahi kumkuta Rais anadhurura Kariakoo, uliwahi mkuta Magomeni anazunguka?,” alisema Majaliwa huku akibainisha kuwa rais ana ratiba nyingi na hatoki hadharani kila mara.