November 24, 2024

Mambo ambayo hutakiwi kufanya wakati wa sikukuu ya Pasaka

Ni pamoja na matumizi ya pesa nje ya bajeti, unywaji wa pombe uliopitiliza na kuvunja amani na utulivu.

  • Ni pamoja na matumizi ya pesa nje ya bajeti, unywaji wa pombe uliopitiliza na kuvunja amani na utulivu.

Dar es Salaam. Huu ni msimu wa sikukuu ya pasaka, kila mtu ana jinsi yake ya kusherehekea sikukuu hii muhimu kwa waumini wa dini ya Kikristo duniani.

Pasaka ni siku muhimu kwa wakristo ambapo wanasherehekea ufufuko wa Yesu kristo baada ya mateso ambapo wanaamini ni kiashilia cha ukombozi wa kiroho wa mwanadamu.

Katika kipindi hiki Wakristo huingia na kutoka katika nyumba za ibada ili kutafakari kuhusu maisha yao na kujumuika na familia, ndugu na marafiki majumbani. 

Hata hivyo, katika kipindi cha furaha, yapo mambo ambayo watu wanatakiwa kujiepusha nayo ili kuhakikisha Pasaka inakuwa njema na mambo mengine yaendelee. 

Haya ndiyo mambo ambayo hutakiwi kuyafanya wakati wa sikukuu ya Pasaka:

Epuka pombe inaweza kukusababishia ajali ya barabarani. Picha|Autocar Professional. 

Epuka unywaji wa pombe uliopitiliza

Baadhi ya watu hutumia mapumziko ya sikukuu kwenda kwenye maeneo ya starehe na kupata vinywaji vikali vya aina mbalimbali. Wengine hunywa pombe kupita kawaida, kulewa na hata kupoteza fahamu na uwezo wa kujisimamia.

Pombe inaweza kukuletea madhara mbalimbali ikiwemo kupata ajali za barabarani na hivyo kuleta ulemavu, majeraha na hata kifo. Umakini unahitajika sana kipindi hiki ili kuepuka madhara kama hayo.

Uvunjifu wa amani na utulivu

Kutokana na baadhi ya watu kuwa na furaha iliyopitiliza, wanaweza kutumia kipindi hiki kufanya vurugu na matendo yasiyofaa ambayo yanaweza kuhatarisha utulivu na amani kwenye jamii.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi Tanzania tayari limetoa tamko kuwa litahakikisha linaimarisha ulinzi kwa raia wote na mali zao kipindi cha sikukuu ya Pasaka.

“Makamanda wa Polisi wa mikoa na vikosi wameshajipanga vizuri kuhakikisha hali ya usalama inaendelea kuimarika na kuwachukulia hatua watakaovunja sheria za usalama barabarani katika kipindi hiki.

“Hiyo ni kwa sababu makao makuu ya polisi imeshawapatia maelekezo na mikakati ambayo kila mmoja ataitekeleza kulingana na mazingira ya eneo lake na mipango ya kamati za usalama za himaya husika,” imeeleza taarifa iliyotolewa jana Aprili mosi, 2021 na Msemaji wa jeshi hilo, David Misime.

Kama ilijipanga kufanya uharifu ni vema ukafikiria mara mbili kabla hujaingia kwenye matatizo ya kuchukuliwa hatua za kisheria.


Soma zaidi:


Epuka matumizi ya pesa yasiyo ya lazima

Ni kweli sikukuu ni kipindi cha furaha na pesa inatumika kukamilisha shughuli mbalimbali ikiwemo kununua chakula na vinywaji. Lakini angalia urefu wa mfuko wako na epuka kuzielekeza fedha zako kwenye matumizi yasiyo ya lazima ikiwemo kununua vitu vya gharama kubwa kuliko uwezo wako.

Mambo ya msingi ni kununua chakula chako na familia yako,  si kulewa na kutoa ofa zisizo na msingi wowote.  Epuka matumizi hayo kwani kesho utakuwa unajuta kwa kutumia pesa nyingi nje ya bajeti.

Hata hivyo, katika kipindi cha mapumziko ya Pasaka kitumie kutafakari hatua uliyopiga kimaisha na kutafuta njia zitakazokusaidia kufikia malengo yako kabla mwaka huu haujaisha.

Pia jumuika na familia yako na mfurahi pamoja na ikiwezekana kaeni nyumbani ili kuepuka changamoto mnazoweza kupata mkitoka mtoko.

Tuambie wewe umepanga kufanya nini sikukuu ya Pasaka? Tutumie maoni yako kupitia WhatsApp: +255 677 088 088.