October 8, 2024

Mambo matatu yatakayosaidia kumaliza Corona Afrika

Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya kiuchumi kwa ajili ya Afrika (UNECA) imependekeza njia tatu kwa mataifa 20 tajiri duniani (G-20) za kuzisaidia nchi za Afrika ikiwemo Tanzania katika vita dhidi ya mlipuko wa virusi vya Corona

  • Ni nchi za G-20 kutoa misaada ya kibinadamu na kuadhinisha mikakati ya kuokoa uchumi wa Afrika.
  • Pia kuwezesha shughuli za uzalishaji na biashara ziendelee kama kawaida kuwapatia kipato raia kwa ajili ya kuishi. 

Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya kiuchumi kwa ajili ya Afrika (UNECA) imependekeza njia tatu kwa mataifa 20 tajiri duniani (G-20) za kuzisaidia nchi za Afrika ikiwemo Tanzania katika vita dhidi ya mlipuko wa virusi vya Corona (COVID-19) ikiwemo kusaidia kuimarisha miundombinu ya afya na kutoa msaada wa moja kwa moja kwenye vituo vilivyopo.

Kamisheni hiyo imesema nchi za Afrika zinajiandaa kwa athari mbaya zaidi za janga hilo lakini zinahitaji msaada kujiandaa kwa janga la kiafya na athari za kiuchumi.

“Hili ni janga la kimataifa lakini Afrika itaathirika zaidi ikibeba mzigo mkubwa na wa muda mrefu wa gharama za kiuchumi ambazo zitatishia hatua zilizopigwa, kuongeza pengo la usawa na kuzidhoofisha zaidi,” imesema taarifa ya UNECA iliyotolewa jana Machi 30, 2020.

Imeeleza kuwa hatua zilizochukuliwa na nchi zilizoendelea za kujiepusha na mikusanyiko na kunawa mikono kila wakati itakuwa changamoto kwa nchi ambazo uunganishwaji wa teknolojia ya intaneti ni mdogo, zenye idadi kubwa ya watu, hazina fursa sawa za upatikanaji wa maji na fursa ndogo ya hifadhi ya jamii.

Ili kuhakikisha nchi za Afrika haziathiriki kiuchumi, kamisheni hiyo imetoa mapendekezo matatu kwa nchi za G-20 kutoa msaada wa haraka kwa mahitaji ya kibinadamu

“Viongozi wa G-20 ni lazima wasaidie na kuchagiza ufunguaji wa njia za biashara hususan kwa makampuni ya madawa na vifaa tiba vingine, lakini pia kusaidia kuimarisha miundombinu ya afya na kutoa msaada wa moja kwa moja kwenye vituo vilivyopo,” imeeleza taarifa hiyo. 


Zinazohusiana


Pia nchi za G-20 zinapaswa kuidhinishwa mara moja mpango wa dharura wa kujikwamua kiuchumi kwa nchi za bara hilo. 

Kwa mujibu wa kamisheni hiyo, viongozi wa G-20 wanatarajiwa kutangaza dola bilioni 100 kufadhili hatua za haraka kwa maeneo kama ya afya , hifadhi ya jamii, kuwalisha watoto walio nje ya shule na kulinda ajira katika bara hilo. 

Kamisheni hiyo pia imesisitiza kuwa msaada huu utolewe kutokana na matarajio, uwazi na uwajibikaji ili mawaziri wa fedha waweze kupanga ipasavyo na asasi za kiraia zinaweza kufuatilia hilo na kuhakikisha kwamba fedha zinatumika kusaidia wale wanaozihitaji zaidi.

UNECA inataka hatua kwa ajili ya kusaidia uingizaji na usafirishaji bidhaa za kilimo, sekta ya madawa na enki pia zinapaswa kuimarishwa ili kuwezesha  mikopo ya muda mrefu na kusaidia kuinua kipato cha wananchi.

Kwa mujibu wa UNECA upatikanaji wa fedha hizi ni muhimu sana ili sekta binafsi ziendelee kufanya kazi , ikiwemo biashara ndogo na za wastani ambazo zinategemea biashara.

Hata hivyo, kamisheni hiyo imesema mipango ya kitaifa na kikanda ya kufufua uchumi inapaswa kujumuisha hatua za kusaidia biashara za Afrika, kuruhusu kusitishwa kwa aina mbalimbali za malipo ikiwemo madeni.