Mambo muhimu ya kutekeleza kabla hujaondoka duniani
Ni kupata muda wa peke yako ili kufikiri na kutafakari tofauti na ulivyozoea. Hii itakusaidia kupata mawazo mapya ya kuendesha maisha yako.
- Ni kupata muda wa peke yako ili kufikiri na kutafakari tofauti na ulivyozoea.
- Pata muda wa ukiwa kwenye mazingira tofauti ikiwemo ufukweni, nyumbani, safarini.
- Hii itakusaidia kupata mawazo mapya ya kuendesha maisha yako.
Ni ukweli usiopingika kuwa kujenga mahusiano mazuri na watu wanaokuzunguka ni jambo muhimu, hasa familia yako ili kuimarisha upendo na furaha ambayo huwezi kuipata kwa watu wengine.
Hata hivyo, maisha ni zaidi ya familia. Kuna wakati unahitaji muda wa kukaa pekee yako na kutafakari mustakabali wa maisha yako kabla hujaondoka duniani.
Baadhi ya tafiti zinaeleza kuwa Unapofanya kitu pekee yako, unaweza kwenda kwa kasi yako mwenyewe na kuongeza ubunifu. Unafikiri na kutafakari tofauti na ulivyozoea, unagundua vitu vipya juu yako mwenyewe, na kuboresha kujiamini kwako.
Pamoja na mahusiano yote ambayo unaweza kuwa nayo katika maisha yako, ni muhimu kujitengenezea muda wa pekee yako. Ukiwa mwenyewe fanya mambo haya angalau mara moja katika muda unaoishi duniani:
Tembelea maonyesho na makumbusho
Tenga muda wako, tembelea maonyesho mbalimbali ya bidhaa na huduma au makumbusho ya Taifa yenye kumbukumbu za historia ya nchi yako na hata dunia.
Hapa nenda peke yako hata kama ni mbali na makazi yako, bila mtu kukushurutisha. Pata muda wa kutosha kuangalia kinachoendelea na kujifunza kwa namna ya tofauti kuliko ile uliyoizoea.
Kutembelea maoneo haya kunategemea na nini unapendelea katika maisha. Kama wewe ni mpenzi wa kazi za sanaa, basi tafuta makumbusho au maonyesho yenye kazi hizo ili kujionea ubunifu na kazi za watu wengine.
Magari yaliyotumiwa na viongozi wa Serikali wa awamu ya kwanza yanayopatikana katika Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Salaam. Picha|Mtandao.
Angalia nyota na anga
Hili unaweza kulifanya wakati wa usiku. Toka nje ya nyumba yako tafuta eneo lenye utulivu, inua macho yako juu uone uzuri wa nyota na mng’ao wake.
Zoezi hili pia litakupa kutafakari kwa namna ya tofauti hasa kuona uumbaji wa asili. Wakati mwingine akili zetu zimekuwa zikochoka na kushindwa kufikiri inavyotakiwa kwa sababu tunawaza kesho yetu itakuaje.
Lakini ukiipa akili muda wa kupumzika na kuona vitu tofauti, utaibua jambo jipya jema katika maisha yako.
Chochea kipaji na karama iliyopo ndani yako
Licha ya kuwa kazi ni muhimu kutupatia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha, lakini tunahitaji kuamsha vipaji vilivyopo ndani mwetu.
Kama unapenda kupiga kinanda au gitaa, kuimba, kuchora au kufanya chochote kinachokupa furaha, basi tafuta muda wa pekee yako na kifanye. Furaha unaitafuta mwenyewe, haitakuja hivi hivi.
Kama kusoma vitabu ni burudani kwako, soma kwa bidii, kwa sababu kipaji ulichopewa kinaweza kukuletea faida kubwa katika maisha na hata kukuingizia kipato.
Zinazohusiana:
- Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako
- Utaoa, utaolewa lini: Jinsi unavyoweza kukabiliana na msukumo wa nje wa ndoa
- Mambo ya kufanya wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka
Angalia watu wanayofanya
Beba maji au juisi yako nenda mahali katika mji ambao wenye mkusanyiko wa watu wengi wanaotembea kwa miguu. Tafuta eneo ukalokaa na kuwaona vizuri mienendo yao.
Kaa hata saa nzima, huku mawazo yako yakitafakari wanachofanya watu wa eneo husika. Utajifunza mambo mengi ikiwemo watu wanavyohusiana na jinsi inavyokupasa kuishi nao unapokuwa katika mkusanyiko wa watu.
Wakati mwingine, tunashindwa kuishi na watu vizuri kwa sababu hatujui tabia zao vizuri.
Jifunze lugha mpya
Uzoeshe ubongo wako kujifunza kuzungumza lugha ambayo umekuwa ukipenda kujifunza. Kuna rasilimali nyingi zinazopatikana mtandaoni ambazo zinaweza kukusaidia kujifunza.
Zipo programu mbalimbali zinazotoa kozi fupi za lugha mbalimbali duniani kama Zinaweza kukusaidia kujifunza taratibu katika muda wako wa ziada.
Nenda ufukweni
Tafuta siku moja ukiwa pekee yako nenda kwenye ufukwe wa bahari au ziwa, tumia muda wako kutembea bila viatu. Miguu yako uguse mchanga huku ukipata upepo mwanana na sauti za mawimbi.
Utajisikia wa tofauti maana hii ni njia mojawapo ya kuondoa msongo wa mawazo na kuipa akili kufikiri tofauti na kupata mawazo mapya ya maisha.
Pia ukiwa ufukweni, unaweza kutumia muda wako kusoma vitabu au kuangalia shughuli zinazoendelea baharini.
Kukaa peke yako kuna faida hasa kama unapata upepo na hewa nzuri inayokufanya ufikiri tofauti na ulivyozoea. Picha|Mtandao.
Panga upya vitu vya nyumbani
Kama unaishi peke yako, chagua siku moja ambayo utafanya shughuli za nyumbani ili kupanga vitu vyako ili kupata muonekano wa tofauti na uliouzoea.
Unaweza kusafisha nyumba, kufua na hata kujipikia chakula kizuri ukipendacho. Lakini pata muda mrefu wa kupumzika ukiwa pekee yako bila kuingiliwa na mtu na hata simu.
Tembelea mazingira ya asili
Tafuta eneo lenye uoto wa asili kama milimani au msituni ambako kuna usalama wa wewe kukaa peke yako. Kaa huko kwa muda huku ukitembea na kujionea fahari ya dunia.
Mazingira tulivu yatakufanya ujisikie vizuri kwa kuvuta hewa safi inayohitajika mwilini.
Mambo haya yanaweza kukusaidia katika kubadilisha maisha yako na kukufanya ujione wa tofauti kila siku. Maisha ni zaidi ya kazi. Maisha ni wewe.
Hata hivyo, wakati ukiwaza kwa ajili yako usiwasahau wengine ambao wamekuwa wakikupa furaha na amani kila siku.