November 24, 2024

Mambo ya kushangaza kuhusu pasipoti yako ya kusafiria

Rangi ya pasipoti yako inatoa taarifa nyingi zaidi unavyofikiria ikiwemo utambulisho wa kisiasa na jiografia wa nchi husika.

  • Rangi ya pasipoti yako inatoa taarifa nyingi zaidi unavyofikiria ikiwemo utambulisho wa kisiasa na jiografia wa nchi husika. 
  • Rangi ya pasipoti ni ufahari na upekee wa nchi katika nyanja za historia na tamaduni za watu wake. 
  • Pasipoti ni zaidi ya rangi, inaweza kuwa fursa au kuzuizi kwa watu kuifikia dunia.

Huenda umekuwa miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakitumia usafiri wa ndege kusafiri katika maeneo mbalimbali duniani, lakini hujagundua jambo moja la kutofautiana kwa rangi za pasipoti kutoka nchi moja hadi nyingine. 

Utofauti wa rangi za pasipoti una maana kubwa na unatumika kama kiwakilishi cha nchi fulani na mambo mengi kuihusu nchi husika. Rangi hutumika kama kitambulisho ambacho huelezea kwa kina kuhusu jambo fulani. 

Pamoja na kutofautiana kwa rangi za pasipoti duniani, pasipoti hizo zinaangukia katika makundi manne tu yaani rangi ya kijani, bluu, nyekundu na nyeusi zenye muonekano tofauti wa vivuli (shades)

Kutofautiana kwa rangi za pasipoti hukuondoi vitu vya msingi na vinavyofanana vinavyohitajika kuwepo kwenye pasipoti zote duniani.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), hakuna kanuni inayolazimisha nchi kutumia aina fulani ya rangi ya pasipoti lakini pasipoti iliyokamilika inatakiwa iwe na vitu vya msingi vinavyoweza kusomwa na mashine (machine readable travel documents -MRTDs) ikiwemo jina na tarehe ya kuzaliwa ya mwenye pasipoti. Ni sababu gani hutofautisha rangi za pasipoti za nchi mbalimbali duniani? 

Sababu za kisiasa na geografia 

Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) zinatumia pasipoti za rangi ya tamu ya mzee iliyokolewa (burgundy color) ambayo ina mchanganyiko na rangi nyekundu. Nchi za jumuiya ya Caribbean zinatumia zaidi rangi ya bluu huku China na Urusi zinatumia nyekundu.

Muonekano wa pasipoti zinazotumiwa na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Picha|Mtandao.

Inaelezwa kuwa rangi nyekundu  inawakilisha historia ya ukomonisti duniani wakati bluu ni kitambulisho kipya cha ulimwengu wa nchi za Amerika ya Kusini na Kaskazini. 

Umuhimu wa kidini

Kwa wengine, matumizi ya rangi za pasipoti huegemea zaidi kwenye dini zao ambazo ni sehemu ya tawala zao. Kwa mfano nchi nyingi za Kiislamu ikiwemo Morocco, Pakistan na Saudi Arabia zinatumia pasipoti za kijani lakini zenye uzito tofauti za vivuli (shades).

Inaaminika kuwa rangi ya kijani ilikuwa inapendelewa zaidi na Mtume Muhammad kama alama inayopambanua ‘asili na maisha’ na rangi hiyo inapatikana pia katika bendera za nchi za Afghanistan na Iran. 

Pia zinatumiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) ikiwemo Niger na Senegal.


Soma zaidi: Kwanini kuna watumiaji wachache wa pasipoti katika huduma za kifedha?


Upekee na kujitofautisha na wengine

Kujitofautisha na kuonekana wa pekee hutegemea vile unavyofanya mambo yako ya kila siku. Hata katika utengenezaji wa pasipoti kila nchi hujaribu kujitofautisha na nchi zingine ili kutambulika haraka na kubaki katika ramani ya dunia. 

Kwa mfano, pasipoti ya Switzerland ina rangi nyekundu inayong’aa, wakati Singapore inatumia rangi ya nyekundu huku anayetumia pasipoti ya muda ya Canada inayotumika kwa dharura inakuwa na rangi nyeupe. 

Pasipoti ya Marekani imekuwa ikipitia mabadiliko kadhaa ya rangi kutoka nyekundu, kijani na sasa ni bluu, ikiwa ni hatua ya kuimarisha utambulisho wake duniani. 

Muonekano wa nje wa pasipoti inayotumiwa Marekani. Picha|Mtandao.

Upatikanaji wake

Uchaguzi wa rangi ya pasipoti japo unategemea zaidi sababu za kihistoria na kitamaduni; pia inategemea upatikanaji wake. Mchakato wa utengenezaji pasipoti unakuwa chini ya udhibiti mkali wa mamlaka na kampuni chache duniani zilizopewa tenda ya kuzitengeneza. 

Inaelezwa kuwa karatasi zinazotumika kutengeneza pasipoti zinasafirishwa na mtu wa tatu (third supplier)  na zinatolewa kwa aina fulani ya rangi ili kukidhi viwango vinavyotakiwa kwa wakati husika. 

Usalama na usafi

Pasipoti ya rangi nyeusi inasifika zaidi kwa kutoonyesha uchafu kirahisi na inachukuliwa kama yenye hadhi ya kiofisi au rasmi (more official). Baadhi ya nchi zinazotumia pasipoti hiyo ni pamoja na Botswana, Zambia na New Zealand  japo kwa sasa, pasipoti nyeusi zinachukuliwa kama miongoni mwa rangi muhimu za Taifa. 

Wakati pasipoti zikiwa na muonekano na rangi tofauti, zinawakilisha kitu kikubwa zaidi kuliko mahusiano ya kisiasa na kiuchumi baina ya nchi. Kwa wengine ni fursa au kizuizi cha kuyafikia maeneo mbalimbali duniani.