Mambo yatakayokusaidia kupunguza hatari ya kupata saratani
Mambo hayo ni pamoja na kubadili mfumo wa maisha, ulaji mzuri wa chakula na kufanya mazoezi.
- Mambo hayo ni pamoja na kubadili mfumo wa maisha, ulaji mzuri wa chakula na kufanya mazoezi.
- Kupima afya mara kwa mara kutakusaidia kujua afya yako na kupata matibabu mapema.
- Watoto wa kike wasicheleweshwe katika kupewa chanjo ya virusi vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi.
Dar es Salaam. Katika kuadhimisha siku ya saratani duniani, Watanzania wameshauriwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kubadili mfumo wa maisha na kupima afya zao mara kwa mara ili kukabiliana na ugonjwa huo na kupunguza gharama za matibabu.
Februari 4 kila mwaka ni siku ya saratani duniani ambayo inaadhimishwa kwa kampeni mbalimbali pamoja na utoaji wa elimu na vipimo kwa wananchi ili kuisadia jamii kujilinda dhidi ya magonjwa ya saratani.
Akizungumza leo jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kila mwaka takribani watu 55,000 hugundulika na saratani ambapo asilimia 52 hufariki dunia. Hiyo ni sawa na kusema kwa kila watu 1000 nchini, mmoja hugundulika kuugua ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Mwalimu, kumekuwa na ongezeko la magonjwa yatokanayo na saratani ambapo saratani ya mlango wa kizazi inaongeza kwa asilimia 31.2 ikifuatiwa na matiti (asilimia 12.9) na saratani ya koo (asilimia .8).
Hata hivyo, Wataalamu wa masuala ya afya wamewashauri Watanzania kuchukua hatua mbalimbali kujilinda na saratani ili kuepusha gharama kubwa za matibabu wakati ugonjwa umefikia hatua ya mwisho.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk Crispin Kahesa amesema bado watu wengi wana dhana potofu kuhusu ugonjwa huo jambo linalosababisha vifo vingi ambapo asilimia 20 tu ndiyo wanaenda hospitali kupata matibabu.
Amesema saratani inatibika na ni vema watu wajitokeze kupima afya zao ili kupata matibabu na chanjo kwa wakati ili kupunguza hatari ya kupata saratani hasa ya shingo ya kizazi.
“Wengi wanakuja hospitali wakiwa wamechelewa huku wengine wakihusisha na tamaduni pamoja na uelewa mdogo kuhusu ugonjwa huo, hivyo rai yangu wajitokeze mapema, saratani inaweza kutibika unapoiwahi,” amesema Dk Kahesa.
Kupima na kutambua hali ya afya yako kunasaidia kupunguza hatari ya kupata saratani na gharama kubwa za matibabu wakati wa ugonjwa. Picha| Mtandao.
Kwa wanawake wenye watoto wachanga wajitahidi kunyonyesha na kujichunguza mara kwa mara kupunguza hatari ya kupata maambukizi ya saratani ya matiti ambayo imekuwa ikiwatesa wanawake wengi duniani.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) saratani inakadiriwa kuua watu milioni 9.6 mwaka 2018 sawa kusema kwa kila watu sita waliofariki basi mmoja alikuwa na saratani.
Dk Kahesa amesisitiza kuwa jambo la muhimu ni watu hasa vijana kubadili mfumo wa maisha ikiwemo kuachana na uvutaji sigara unaowaweka katika hatari ya kupata saratani ya mapatu ambayo inashambulia mfumo wa upumuaji.
Pia kuzingatia ulaji wa vyakula vyenye virutubisho ikiwemo matunda, mbogamboga kwa wingi pamoja na maji ya kutosha na kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi zikiwemo chipsi na chama.
Sambamba na hilo ni kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ya mwili ili kutoa taka au sumu zisizohitajika mwilini na kuufanya mwili kuwa katika muonekano mzuri na uzito unaohitajika kwa kila umri wa binadamu.