October 7, 2024

Mamlaka Arusha zaelezea undani kukamatwa kwa wanahabari wa Kenya

Wanahabari wawili kutoka Kenya wanashikiriwa na mamlaka mkoani Arusha wakituhumiwa kuingia nchini na kufanya shughuli za uandishi bila kibali na muda wowote wiki hii watafikishwa mahakamani.

  • Zasema waliingia nchini kwa njia za panya wakiwahoji wananchi kuhusu Corona.
  • Wakabidhiwa kwa Uhamiaji kwa ajili ya taratibu za kisheria, kufikishwa mahakamani wiki hii.

Dar es Salaam. Wanahabari wawili kutoka Kenya wanashikiriwa na mamlaka mkoani Arusha wakituhumiwa kuingia nchini na kufanya shughuli za uandishi bila kibali na muda wowote wiki hii watafikishwa mahakamani.

Mkuu wa Wilaya ya Longido Frank Mwaisumbe ameiambia Nukta kuwa wanahabari hao walikamatwa Jumamosi Saa 7:30 mchana wakiwahoji wakazi wa maeneo hayo kuhusu masuala ya ugonjwa wa virusi vya corona.

“Tuliwakamata Wakenya wawili ambao walijitambulisha kuwa ni wanahabari kutoka Elimu TV na walikuwa na camera na vifaa vingine vya kurekodia. Hawakuingia nchini kwa kufuata taratibu za uhamiaji pale mpakani na wala hawakuwa na kibali cha kufanya uandishi kutoka TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania),” amesema Mwaisumbe.

Amesema mamlaka zinawachukulia hatua na wiki watakifikishwa mahakamani kwa kuingia nchini bila kufuata taratibu na kufanya kazi zao bila kibali.


Soma zaidi: 


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Jonathan Shanna amewataja wanahabari hao kuwa ni mpiga picha Clinton Isimbu (22) na mwanahabari Kaleria Shadrack mwenye miaka 23.

Watuhumiwa hao, kwa mujibu wa Kamanda Shanna wameshakabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji mkoani humo kwa ajili ya taratibu nyingine za kisheria.