Maoni mchanganyiko kanuni mpya kusimamia vifurushi vya simu Tanzania
Baadhi yao wamesema zitawapatia ahueni ya kuongezeka kwa gharama za vifurushi ambavyo vinaisha kabla ya muda uliowekwa.
- Ni kanuni ndogo za kuratibu utoaji wa huduma za vifurushi vya mawasiliano ya simu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
- Kanuni hizo ni kwa ajili ya kutatua malalamiko ya makato yasiyo sahihi ya gharama za matumizi ya vifurushi vya simu za mkononi.
- Baadhi yao wamesema zitawapatia ahueni ya kuongezeka kwa gharama za vifurushi ambavyo vinaisha kabla ya muda uliowekwa.
Dar es Salaam. Baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutangaza kanuni mpya zitakazosimamia vifurushi vya simu nchini, Watanzania wamekuwa na maoni tofauti huku baadhi yao wakisema zitawapatia ahueni ya kuongezeka kwa gharama za vifurushi hivyo.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, Machi 2, 2021 alisema mamlaka hiyo imetengeneza kanuni ndogo za kuratibu utoaji wa huduma za vifurushi vya mawasiliano ya simu ikiwa ni hatua ya kutatua malalamiko ya makato yasiyo sahihi ya gharama za matumizi ya vifurushi vya simu za mkononi.
Kanuni hizo zitasimamia vifurushi vya dakika za kupiga simu, bando la intaneti na meseji zinazotumwa kwenye simu za mkononi nchini Tanzania.
Utekelezaji wa kanuni hizo utaanza Aprili 2 mwaka huu ambapo miongoni mwa yanayoelekezwa kwenye kanuni hizo ni huduma zote za vifurushi lazima zipate vibali vya TCRA ambapo mamlaka hiyo imetoa mwongozo wa bei za vifurushi zinazotakiwa kutekelezwa na kampuni za simu.
Kampuni za simu hazitatoa huduma za vifurushi bila kibali cha TCRA na kuhakikisha bei za vifurushi zinazingatia bei husika ya chini na ya juu zilizowekwa na mamlaka hiyo, kutumia lugha rahisi, vigezo na masharti yaliyo wazi kuhusu vifurushi vinavyotolewa.
“Vifurushi vinavyotolewa kwa Mtumiaji havitaondolewa, havitarekebishwa au kubadilishwa ndani ya miezi mitatu baada ya kuidhinishwa.
Mtoa huduma atatoa fursa kwa Mtumiaji wa huduma za mawasiliano kuchagua na kujiunga na vifurushi visivyokuwa na ukomo wa muda wa matumizi vitakavyo patikana kwenye menyu kuu na watatumia jina linalofanana kwa vifurushi hivi ili vitambulike kwa wepesi,” inaeleza sehemu ya kanuni hizo.
Mtoa huduma atatoa taarifa kila wakati matumizi ya kifurushi yatakapofikia asilimia 75 na 100 kwa vifurushi vya muda wa maongezi, data na sms.
Pia, mtoa huduma hatafanya promosheni zaidi ya tatu au kutoa ofa maalum zaidi ya tatu kwa wakati mmoja kupitia huduma za sauti, sms na data.
Kwa wengine, kanuni mpya za TCRA zitakapoanza kufanya kazi, zitawezesha usawa miongoni mwa watoa huduma na Watanzania. Picha| Wallpaperflare.
Watanzania watoa maoni kuhusu kanuni hizo
Baada ya TCRA kutangaza kanuni hizo kumekuwa na maoni tofauti kwa Watanzania hasa wale wanaotumia mitandao ya kijamii ikiwa kama zitasaidia kutatua changamoto na malalamiko yao kuhusu vifurushi vya simu.
Miongoni mwa malalamiko hayo ni kuongezeka kwa gharama za vifurushi ambavyo vinaisha mapema kabla ya muda kuisha.
Mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Mediatrice Raphael amesema kwake kuongezeka kwa gharama za vifurushi kumemuathiri hadi katika gharama zake za maisha hasa ikizingatiwa kuwa anafanikisha masomo yake kwa nguvu ya mkopo.
“Nilkuwa natumia Sh1,000 napata Gb1 na dakika 100 kwa wiki moja baada ya miezi mitatu wakapandisha ikawa Sh3,000 napata Gb1.1.” amesema mwanafunzi huyo akibainisha kuwa anatarajia kanuni hizo mpya zimrudishe katika gharama zake za awali.
Kwa wengine, kanuni mpya za TCRA zitakapoanza kufanya kazi, zitawezesha usawa miongoni mwa watoa huduma na Watanzania kwani zimezingatia manufaa kwa pande zote mbili.
Mjasiriamali jamii Abel Kyalaaliko amesema TCRA imefanya jambo jema kudhibiti vifurushi vya simu kwa sababu baadhi ya kampuni za simu hufidia gharama zinazopotea katika promosheni za mitandao yao au kampeni zingine wanazoingia kupitia vifurushi vya data kwa sababu vifurushi vya dakika na SMS havitumiwi sana.
Kyalaaliko amesema anakubaliana na sharti la mtoa huduma asitoe huduma za vifurushi bila kibali cha TCRA.
“Kanuni mpya zimeangalia kunufaisha pande zote mbili. Mfano kanuni ya kumwezesha mtu aliyejiunga kuendelea kutumia uniti zilisosalia kwa kununua kingine, wamewezesha mauzo ya watoa huduma huku ikimlinda mtumiaji kutoweza kupoteza kifurushi chake hewani,” amesema Kyalaaliko wakati akiongea na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) .
Soma zaidi:
- TCRA yatangaza kanuni kudhibiti vifurushi vya simu Tanzania
- Mambo ya kuzingatia unapotumia Uber, Taxify
- Teknolojia ya utengenezaji mkaa mbadala inavyoweza kupunguza ukataji miti ovyo
Kanuni hizo pia zitaendelea kuwa msaada kwa wafanyabiashara ambao wanaendesha shughuli zao mtandaoni na kufanya vifurushi vya intaneti kuwa muhimu katika biashara zao.
Kwa mfanyabiashara wa mtandaoni wa Mkoani Dar es Salaam, Zipporah Zealot, amesema kilichomvutia ni kipengele cha kumwezesha mtu kuhamisha bando la intaneti kwa mtu mwingine kabla muda kuisha.
“Watu wengi sana tutanufaika apo! Tungependa walifanyie kazi hili jambo la vifurushii kupanda bei bado ni mtihani mzito kwa jamii tunaomba sana walifanyie kazi, ili bei za vifurushii ziwe nafuu,” amesema Zealot.
Wakati wadau hao wakizungumza moja kwa moja na Nukta Habari, wadau wengine wametoa maoni yao kwa njia ya mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter na Instagram wakijadili kwa mapana kuhusu suala hilo.
Mkurugenzi na mwanzilishi wa programu tumishi ya simu ya elimu ya Mtabe na jukwaa mtandaoni la My Elimu, Given Edward amesema taarifa ya kupungua kwa gharama za mawasiliano bila kununua bando haiendani na uhalisia kwani Watanzania wengi wanatumia bando za intaneti na huko ndiko gharama zimeongezeka.
Given ambaye ni mtaalam wa mifumo ya teknolojia ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwa, “waelezee tu sababu nzuri za kupandisha. Ila sio kusema kwamba gharama hazijapanda. Watu sio wajinga hivyo. Tunatumia hizi bando kila siku. Tunazilipia hizi bando kila siku. Pale tunachokilipia kinapobadilika, tunafahamu.”
Wafanyabiashara wa mandaoni wamefurahishwa na kipengele cha kumwezesha mtu kuhamisha bando la intaneti kwa mtu mwingine kabla muda kuisha. Picha| Mea Markerts.
Wadau wengine wa simu za mkononi Tanzania wamesema kanuni hizo zitasaidia kudhibiti kubadilika kwa huduma ya vifurushi bila kutolewa taarifa kwa watumiaji.
“Kuna bando lao la SMS bila kikomo baadaye walibadili bila taarifa tukajikuta kuna kikomo cha meseji za kutuma. Bila taarifa,” amesema mdau aliyejulikana kwa jina moja la Peter katika mtandao wa WhatsApp.
Kupitia ukurasa wa TCRA wa Instagram, Watanzania pia wametoa ya moyoni wakisema ni vyema suala la kutumia bando hadi kuisha ni muhimu kuzingatiwa.
“Uniti za umeme nazo tungekuwa tunapangiwa muda ingekuaje? Yanatakiwa yaondoke haya makandamizo. Umenunua kifurushi cha elfu, utumie mpaka kiishe sio utumie ndani ya masaa fulani unakuwa ni wizi,” amesema @sharif_bayona katika mtandao wa Instagram.
Wewe unazionaje kanuni mpya za TCRA unafikiri ni mwarobaini wa changamoto za vifurushi vya simu nchini? Toa maoni yako kupitia mitandao yetu ya kijamii @NuktaTanzania kupitia mtandao wa Facebook, Instagram na Twitter.