November 24, 2024

Maoni mchanganyiko kuruhusiwa shughuli za utalii Tanzania

Dk Kigwangalla kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema maagizo yaliyotolewa na Rais ni mwongozo utakaofungua fursa kwa Tanzania kuendelea kufaidika na sekta ya utalii.

  • Rais John Magufuli  ameruhusu watalii waingie nchini bila ya kukaa karantini kwa siku 14.
  • Baadhi wadau wasema itasaidia kuokoa ajira za watu na kuongeza kipato. 
  • Wapendekeza tahadhari za kujikinga ziendelee kuchukuliwa.

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla amesema kuruhusiwa kuingia tena kwa watalii nchini Tanzania ni fursa ya kuimarisha sekta ya utalii na kuiingizia nchi mapato ya kigeni. 

Kwa sasa anga la Tanzania limefunguliwa baada ya jana Rais John Magufuli kuagiza watalii waruhusiwe kuingia nchini ili kujionea vivutio mbalimbali vya utalii. 

Dk Magufuli aliyekuwa akitoa salamu za Taifa katika kanisa la KKKT Chato mkoani Geita alisema baadhi ya ndege tayari zimeanza mipango ya kuwaleta abiria nchini.  

Dk Kigwangalla kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema maagizo yaliyotolewa na Rais ni mwongozo utakaofungua fursa kwa Tanzania kuendelea kufaidika na sekta ya utalii.

“Hotuba imetupa mwongozo mzuri wa kutupeleka mbele. Anga sasa linafunguliwa kwa ndege za abiria, ndege zinaanza kutua,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Dk Kigwangalla.

Pia, waziri huyo amepongeza uamuzi wa Rais Magufuli wa kuondoa ulazima wa wageni wote wanaoingia nchini kukaa karantini kwa siku 14 na wakifika watakwenda moja kwa moja kwenye vivutio vya utalii. 

Hata hivyo, waziri huyo amesema tahadhari zote za ugonjwa Corona zitazingatiwa katika maeneo yote watakayokuwepo watalii hao ili kuwaepusha na maambukizi. 


Zinazohusiana


Baadhi ya wadau wa masuala ya utalii nchini wamesema hatua hiyo itasaidia kupunguza athari zilizojitokeza katika sekta ya utalii ikiwemo kushuka kwa mapato na watu wengi kupoteza ajira.

Muongoza watalii wa mkoani Kilimanjaro Makarious Munisi amesema hatua hiyo itasaidia kuwarudisha kazini kwani dunia nzima imechoka kukaa ndani.

Munisi ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa kwa kipindi ambacho kulikuwa na zuio la safari, takribani asilimia 80 ya ofisi za waongoza utalii mkoani Arusha na Kilimanjaro zilikuwa zimefungwa.

“Kuendelea kubaki ndani siyo suluhisho na inaua sekta ya utalii. Kuruhusu safari kwa sasa ni faida kwani tutapata watalii zaidi ya majirani zetu,” amesema Munisi. 

Mdau huyo wa utalii amesema licha ya watalii kutoka nje, hata utalii wa ndani umeshuka kuliko ilivyowahi kushuhudiwa awali. 

Hata hivyo, amesema inaweza kuchukua muda kwa utalii hasa wa ndani  kurudi kwenye hali yake kwasababu bado uchumi wa watu haujatengamaa na kwa sasa wanaelekeza fedha zao kwenye mahitaji ya msingi. 

“Taasisi zilikuwa zimesitisha mizunguko. Inahitaji muda kujijenga kiuchumi ili zirudi kwenye hali yake,” ameelezea Munisi.