October 7, 2024

Maoni mchanganyiko matumizi fedha za Tasaf Mwanza

Baadhi ya fedha hizo zimekua hazitumiki kwa malengo yaliyokusudiwa kutokana na wanufaika kushindwa kuzitumia katika shughuli za uzalishaji mali.

  • Baadhi ya wanufaika wa mfuko huo hawazitumii kwa malengo yaliyokusudiwa.
  • Ukubwa wa familia na umri mkubwa wachangia hali hiyo. 
  • Wengine wanazitumia katika shuguli za kilimo kuongeza kipato.

Mwanza. Licha ya Serikali kutumia mamilioni ya fedha  kukabiliana na tatizo la umasikini nchini kupitia  Mpango wa Taifa wa Kusaidia Kaya Masikini (Tasaf),  baadhi ya fedha hizo zimekua  hazitumiki kwa malengo yaliyokusudiwa kutokana na wanufaika  kushindwa kuzitumia katika shughuli za uzalishaji mali.

Changamoto  hiyo inatokana na wanufaika  kuwa wenye umri mkubwa,  huku  baadhi yao wakisumbuliwa na magonjwa mbalimbali pamoja na wingi wa watoto  kwenye familia. Inawakumba baadhi ya wanufaika wa Tasaf katika Mkoa wa Mwanza, jambo ambalo linawafanya waendelea kuogelea kwenye umasikini.

John  Mashimba ni mmoja wa wanufaika kutoka mtaa wa National Jijini Mwanza,  anaelezea kiasi cha fedha anachopokea hakiwezi kumsaidia kuongeza  kipato kutokana na idadi kubwa ya familia inayomtegemea. 

“Ninajumla ya watoto saba,  wote ni wanafunzi na wananitegemea,  kiasi cha Sh40,000 ninachopokea hakitoshelezi kukidhi mahitaji na kuanzisha biashara nyingine,” anasema Mashimba.


Soma zaidi: 


Wakati baadhi ya wanufaika wakilalamika, wengine wanajiongeza kwa kuwekeza fedha hizo katika miradi yenye tija kiuchumi. 

Mnufaika mwingine  Kija Saanane pamoja na kuwa na familia ya watoto  tisa wanaomtegemea anarudisha fadhila kwa Tasaf  baada ya ruzuku anayopata kuigawa sehemu mbili. 

“Napokea kiasi cha Sh60,000 naigawa katikati nyingine natumia kwenye shughuli za uzalishaji mali,” anasema Saanane. 

Saanane ambaye ni mjane anasema fedha hizo huzitumia kununulia mbolea kwa ajili ya kilimo cha bustani na mboga mboga,  kufugia kuku na mpaka sasa amefanikiwa kujenga nyumba. 

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Tasaf,  Zuhura Mdungi amesema wanufaika hao bado wana nafasi ya kutumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi. 

Mdungi amesema mbali  na kutegemea fedha  hizo, pia wana wajibu wa kujiunga kwenye vikundi vya kijamii vya kukopeshana ili waweze kujiongezea kipato.