Maoni mchanganyiko wanafunzi kufanya kazi shuleni
Wadau wa elimu wajadili kwa mtazamo tofauti, wanafunzi kufanya kazi ndogo ndogo wakiwa shuleni, baadhi wakikubaliana na dhana hiyo huku wengine wakikataa.
- Baadhi ya wazazi na wadau wa elimu wamesema mtoto akishirikishwa katika kazi ndogo ndogo za shuleni zinasaidia kumjenga na kumfanya kuwa mchapakazi baadaye.
- Wengine wameeleza kuwa lengo la mtoto kwenda ni kusoma na kupata maarifa siyo kufanya kazi.
- Wadau wa elimu wameeleza kuwa mzazi ndiye mwenye jukumu kumfundisha na kumuelekeza mtoto kazi za kufanya.
Dar es Salaam. Mwangaza ni mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Kila siku huamka 12:00 asubuhi kujiandaa kwa ajili ya kwenda shule lakini hatembei kwa miguu kwa sababu gari huja kumchukua nyumbani na kumpeleka shuleni.
Hata akifika shuleni anakuta darasa na mazingira ya shule yake yakiwa safi. Majukumu yake siyo kuhakikisha mazingira anayosomea yanakuwa katika hali nzuri bali kutumia muda unaokuwa shuleni kujisomea ili kuongeza maarifa.
Mwangaza (jina siyo halisi) pia hushiriki michezo siku ya ijumaa baada ya vipindi ili kuchangamsha akili na hata akirudi nyumbani, hupata muda mwingi wa kupumzika, kuangalia televisheni na wakati mwingine kuwasaidia wazazi kwa shughuli ndogo ndogo za nyumbani.
Maisha ya msichana huyo yanawakilisha wanafunzi wengi wanaosoma katika shule za zinazomilikiwa na watu binafsi zinatajwa kuwa zina mazingira bora ya kusomea lakini wanafunzi hao hawapati fursa ya kufanya kazi za shuleni kama kufagia, kumwagilia maua na hata kusafisha vyoo.
Suala hili limekuwa likiibua mjadala kwenye jamii, juu ya mstakabali wa watoto ambao hawapati fursa ya kushiriki kazi za shuleni isipokuwa kwenda shuleni kusoma na kurudi nyumbani.
Baadhi ya watu wamekuwa wakisema mtindo huo wa maisha wa baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule hizo, unawafanya kuwa wavivu, kukosa stadi muhimu za maisha na kushindwa kushiriki kikamilifu shughuli za kijamii wanapokuwa watu wazima.
Maoni na uchambuzi uliofanywa na www.nukta.co.tz kutoka kwa wanafunzi, wazazi pamaja na wataalam wa masuala ya elimu yatakupa picha na nini kilichojificha katika nadharia za wanafunzi kusoma bila kushiriki moja kwa moja katika shughuli za shuleni.
Monalisa Raymond ni mama wa watoto wawili anasema mtoto wake wa kwanza (10) anasoma katika shule moja ya msingi binafsi iliyopo jijini Dar es Salaam mbali na masomo, wanafunzi wa shule hawaruhusiwi kufanya kazi zingine zaidi ya kukaa darasani na kusoma tu.
“Ninapenda watoto wafundishwe kazi. Im not talking about swimming (siongelei kuhusu kuogelea), ninaongelea kazi muhimu kama kufagia na zinginezo,” amesema Mona.
Monalisa anaamini shuleni ni sehemu sahihi ya mtoto kujifunza kufanya kazi, licha ya kuwa mzazi ndiye mwenye jukumu la kumlea na kumfundisha kufanya kazi.
Dhana ya mama huyo ni kuwa wanafunzi wanatumia muda mwingi wakiwa shuleni kuliko nyumbani, na kama shule ina utaratibu wa kuwapa kazi ndogondogo inasaidia kuwajenga kimaadili na kupenda kufanya kazi.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, inaeleza kuwa mtu yeyote haruhusiwi kumuajiri mtoto katika shughuli yoyote inayoweza kuwa na madhara katika maendeleo ya afya, elimu, akili, mwili na maadili yake. Picha| H2O for Life.
Mkazi mwingine wa Boko, jijini Dar es Salaam, Verediana Mwashi, yeye ana mtazamo tofauti juu ya jambo hilo, kwa sababu lengo kuu la kumpeleka mtoto ni ili akasome na si vinginevyo.
Licha ya kuwa mtoto wake anasoma shule ya msingi ambayo wanafunzi hufanya kazi ndogo ndogo zikiwemo za kuokota makopo na kufagia, ameiambia www.nukta.co.tz kuwa kama ni kazi, mtoto anapaswa kufundishwa nyumbani na waalimu waache watimize majukumu yao ya kuwaongezea maarifa wanafunzi.
“Sasa mtoto afike shuleni aanze kufagia mara kudeki, akiingia darasani si ni kusinzia tu. Wengine mara wanachota maji wengine wanalima asubuhi sasa si mtoto anasinzia darasani na masomo yanampita?,” amehoji Mwashi.
Wanafunzi nao wana mtazamo tofauti
Evance William ambaye ni Mwanasheria katika kampuni ya uwakili ya Extent Corporate Advosory anasema akiwa anasoma shuleni hawakuwahi kufanya kazi zozote kwani walikuwepo wafanyakazi walioajiriwa na uongozi wa shule kwa ajili ya usafi na mambo mengine.
Hata hivyo, William amesema kwa umri wake (23) hakuna kazi yoyote ya nyumbani inayomshinda kwa sababu katika kipindi cha likizo, alishiriki kikamilifu kazi za nyumbani.
“Najua kuna watu ambao hata kufanya kazi rahisi hawawezi. Binafsi nina fanya kazi zote kwa sababu wazazi wangu walinifunza tangu ningali mdogo wakati wa likizo,” anasema William.
Zinazohusiana
- Twaweza: Wazazi wengi hawajui matokeo halisi ya shule za watoto wao
- Sababu za wazazi kuwaongoza watoto kusoma vitabu
Wakati William akiamini mzazi ndiye mwenye jukumu la kumfunza mwanafunzi kazi, Linda Amos anasema shule ina sehemu yake kumjenga mwanafunzi kupenda kufanya kazi.
Amos ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCO) anasema licha ya kazi alizojifunza wakati anasoma Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Theresia ya Ukonga jijini Dar es Salaam siyo zote anaweza kuzifanya inavyotakiwa.
“Zipo kazi kama kupekechua mahindi ambazo nyumbani nilikuwa sizifanyi lakini kupitia shule nimefundishwa na nikienda kijijini kusalimia ndugu ninaweza kuzifanya,” amesema Amos.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, inaeleza kuwa mtu yeyote haruhusiwi kumuajiri mtoto katika shughuli yoyote inayoweza kuwa na madhara katika maendeleo ya afya, elimu, akili, mwili na maadili yake.
Kwa mfano, kazi katika viwanda vya kemikali inaleta athari kwa afya ya mtoto. Kazi ya mashambani au machimboni inayozuia mtoto kwenda shule inaathiri elimu, akili na mwili wake.
Pamoja na haki za kulinda ustawi wa mtoto, sheria hiyo inasema mtoto atakuwa na wajibu na jukumu la kufanya kazi kwa ajili ya mshikamano wa familia; kuwaheshimu wazazi, walezi, wakubwa wake na watu wazima muda wote na atawasaidia pale inapohitajika ikiwemo kufanya kazi ndogo ndogo.
Wakati William akiamini mzazi ndiye mwenye jukumu la kumfunza mwanafunzi kazi, Linda Amos anasema shule ina sehemu yake kumjenga mwanafunzi kupenda kufanya kazi. Picha| Mtandao.
Kazi zinamsaidia mwanafunzi kujitegemea
Kwa upande wake, mwalimu wa somo la Jiografia kutoka Shule ya Sekondari Bwawani ya mkoani Pwani, Hamis Juma anasema kazi ambazo wanafunzi wanapewa wawapo shuleni zinawasaidia kuwajenga na kuwafundisha kujitegemea wakiwa watu wazima na hata kujiajiri kwa sababu zinahusisha stadi muhimu za maisha.
“Mtoto anakuwa mkubwa hajui kufanya kazi kwa sasabu tangu awali amezoeshwa kufanyiwa kila kitu. Unaoa msichana kufagia hajui, kupika hajui matokeo yake mnakula vyakula hotelini,” amesema Juma.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wa elimu wanasema kila shule ina utaratibu wake wa kutoa elimu ambao umewekwa kisheria na jukumu la kumfunza kazi mtoto ni la mzazi kuliko shule.
Amos na Monalisa wanasema kuwa mzazi ana sehemu kubwa katika uelimishaji wa mtoto hasa kumfunza jinsi ya kufanya kazi kuliko shule anayosoma.
Mbali na hayo, licha ya waalimu kuwa na wajibu katika malezi ya mtoto, wajibu wa mwalimu ni wa muda mfupi ukilinganishwa na wa mzazi ambaye wajibu wake hudumu muda mrefu.