November 24, 2024

Maoni mchanganyiko ya Watanzania baada ya Diamond kukosa tuzo za BET

Baadhi wampongeza na kumwambia akaze buti huku wengine wakimwamwambia ajirekebishe mapungufu aliyo nayo.

  • Baadhi ya Watanzania wamemtia moyo kuwa asikate tamaa aendele kupambana.
  • Wengine wamesema aboreshe mziki wake ili uendelee kukubalika kimataifa.
  • Diamond amewashukuru Watanzania waliomshika mkono kipindi chote cha tuzo hizo.

Dar es Salaam. Kumekuwa na mirindimo ya maoni tofauti mtandaoni kwa Watanzania baada ya washindi wa tuzo za BET kutangazwa usiku wa kuamkia leo Juni 28, 2021 huku Msanii kutoka Tanzania, Naseeb Abdul almaarufu kama Diamond Platnumz akikosa tuzo hiyo.

Tuzo za BET ni tuzo mashuhuli za wasanii wa muziki ngazi ya kimataifa zinazotambua wanamuziki waliofanya vyema katika tasnia ya muziki kwa ngazi ya makundi, binafsi, albamu na tanzu za muziki kwa mwaka husika.

Tuzo hiyo imeenda kwa msani wa Nigeria, Damini Ogulu a.k.a Burna Boy na kuwabagwa wenzake alioshiriki nao katika kinyang’anyiro cha kumpata “Best International Act” (msanii bora kipengele cha kimataifa).

Burna Boy anatamba na nyimbo zake maarufu zikiwemo “On The Low”, “Wonderful” na “Ye” ambazo zimekuwa zikipokewa kwa namna tofauti duniani. 

Katika tuzo za mwaka huu (2021), Platnumz aliingia kwenye mchuano na wasanii wawili kutoka Nigeria, akiwemo Damini Ogulu (Burna Boy) na Ayodeji Balogun (Wizkid) ambao wamechuana vikali kuwania tuzo ya “Best International Act”.

Wasanii wengine walioingia katika kundi hilo ni pamoja na Emicida (Brazil), Headie One na Young T & Bugsey (Uingereza) na wasanii Youssoupha Kutoka na Aya Nakamura kutoka Ufaransa..

Kilele cha tuzo hizo kimefanyika nchini Marekani katika ukumbi wa Microsoft mjini Los Angeles ambapo washindi wa vipengele vingine walitangazwa.

Katika tuzo hizo Diamond alikuwa mwakilishi pekee kutoka nchi za Afrika Mashariki. Picha| Diamond Platnumz.

Watanzania wazifungukia tuzo hizo

Licha ya kuwa nyota kutoka Tanzania aliyetamba na vibao mbalimbali vikiwemo “Mbagala”, “Waah” na “African Beauty” hatarejea nyumbani na tuzo mkononi, Watanzania wameendelea kumpa moyo wakisema bado ni mshindi na daima kuna awamu nyingine.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Gerson Msigwa kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema, licha ya kuwa tuzo hiyo haijaona ardhi ya Tanzania, kazi itaendelea kwa msanii Diamond Platnumz (Simba).

Msigwa ameandika, “Hatukupata tuzo lakini tumeongeza heshima. Kudos @diamondplatnumz, Watanzania tunajua wewe ni mshindi, mpambanaji, mzalendo wa kweli na mwanamuziki bora sana Afrika na Duniani. Tutaipata wakati mwingine.”

Naye Mariam Ismail (@Mariam38295441) amesema “Platnumz bado ni mshindi”. 

Kwa Mariam, Ushindi wa Platnumz umeanzia kwa msanii huyo kuorodheshwa kama mmoja ya wanaogombea tuzo hiyo, jambo ambalo limeonyesha jinsi gani anavyozidi kupamba katika ngazi za kimataifa. 

“Inaonyesha ni kiasi gani umeupambania mziki wetu na #SwahiliNation kwa ujumla. Hongera sana @diamondplatnumz,” ameandika Mariam katika ukurasa wake wa  Twitter.

Licha ya kukosa tuzo hizo, Diamond amefanikiwa kuutangaza utamaduni wa Tanzania kimataifa baada ya kuvaalia mavazi ya kabila la Wamasai huku akiwa ameshika ngao inayodhihirisha kuwa yuko imara.

Hata wakati baadhi wakimtia moyo Diamond, wengine wamesema kushindwa kwake katika tuzo hizo kuwe chachu ya kuwaunganisha mashabiki wake hasa pale wanapofanyiwa vitendo vilivyo kinyume na haki za binadamu kutoka kwa watawala. 

“Tunaamini umejifunza sana kusimama na wa Tanzania wengi, especially kwenye haki. Zaidi tunqejisikia furaha pia, umetuwakilisha tena kwa namna ya kipekee kabisa. Niwakumbushe tu kuwa Wasanii mna dhamana kubwa sana, ya kuwapigania wasiokuwa na sauti kwa kuwa sauti zenu zinavuma sana,” ameandika Gerison Stephen @gerison_stephen wakati akimjibu @diamondplatnumz katika ukurasa wake wa Twitter. 

Naye Ally Mwandike (@Mwandike) kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema ni muda kwa msanii huyo kuwekeza katika muziki wake na kuacha “janja janja” kama wasanii aliokuwa akishindanishwa nao walivyowekeza. 

“Tuwe wa kweli, kwanza BET wamewakosea sana heshima kina Burna na Wizkid, Diamond siyo wa ngazi sawa na wasanii hawa . Hawa jamaa wamewekeza kwenye muziki mzuri na wanafanya vizuri duniani, Diamond atulize kichwa aanze kutengeneza muziki mzuri bila janja janja,” ameandika Mwandike katika ukurasa huo.

Diamond naye atoa ya moyoni

Baada ya washindi kutangazwa, Diamond Platnumz amesema licha ya kuwa haijaibuka mshindi lakini anawashukuru Watanzania kwa kumpigania na kumfikisha hapo alipofika.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Platnumz amesema tuzo za BET zimemfunza mengi ikiwemo umoja wa Watanzania na upendo.

“Nifarajia kuona dunia inapotaja nchi zenye wanamuziki bora, Tanzania inatajwa, ni jambo la kumshukuru Mungu. Na naamini wakati mwingine tutaibeba, nitafarijika kesho na kesho kutwa msanii mwingine pia akiwa katika jambo la kuwakilisha taifa tumpe nguvu kama mlionipa,” ameandika Platnumz.

 Katika tuzo hizo Diamond alikuwa mwakilishi pekee kutoka nchi za Afrika Mashariki.

Afrika nayoyazungumza

Ushiriki wa Platnumz katika tuzo za BET haukuwa chachu kwa Watanzania pekee bali hata wasanii na wananchi wa mataifa mengine ikiwemo Kenya.

Msanii kutoka Kenya, Kevin Kioko almaarufu kama Bahati amesema Diamond amefanikiwa kufikia hatua kubwa katika umri mdogo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha vijana wengi.

Bahati amesema kupitia Twitter kuwa Platnumz amefanya kazi kubwa ya kuwahamasisha watoto wengi  kuwa unaweza kutokea katika umasikini na ukatoboa kimaisha.