October 6, 2024

Mara yashindwa tena kutoboa mtihani darasa la saba 2019

Imeshika nafasi ya mwisho kitaifa kama ilivyokuwa mwaka jana katika mtihani huo na kuingiza shule moja na halmashauri mbili za Butiama na Rorya kwenye orodha ya halmashauri 10 za mwisho kitaifa.

  • Imeshika nafasi ya mwisho kitaifa kama ilivyokuwa mwaka jana.
  • Imeingiza shule moja na halmashauri mbili za Butiama na Rorya kwenye orodha ya halmashauri 10 za mwisho kitaifa.

Dar es Salaam. Jinamizi la wanafunzi kufeli katika mtihani wa darasa bado linauandama mkoa wa Mara, baada ya kushindwa kujichomoa katika nafasi ya mwisho kitaifa iliyoshikilia mwaka 2018.  Mwaka huu, mkoa huo umeshika tena nafasi ya mwisho kitaifa, jambo ambalo linaibua maswali lukuki juu ya mstakabali wa elimu kwa watoto wa mkoa huo unaopatikana kanda ya ziwa.

Mpangilio wa mikoa kwa ubora wa ufaulu katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2019  unaonyesha kuwa Mara imeshika nafasi ya mwisho kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara sawa na mwaka jana.

Anguko la Mara lilitokea mwaka 2018 baada ya kuporomoka kwa kasi kutoka nafasi ya 13 iliyorekodiwa mwaka 2017 hadi nafasi ya 26. Tangu hapo mkoa huo unajikongaja mkiani tu.


Mkoa huo ulikuwa na wanafunzi 53,233 walioshiriki mtihani wa mwaka huu, ni wanafunzi 35,668 tu wamefaulu mtihani huo.Hiyo ni sawa na kusema takriban wanafunzi saba kati 10 au asilimia 69.7 wamefaulu mtihani huo ukilinganisha na mwaka jana ambapo ilikuwa asilimia  63.68. Lakini katika miaka yote miwili mkoa huo uko chini ya wastani wa kitaifa.

Katika Matokeo ya kumaliza elimu ya msingi yalitangazwa Oktoba 15, 2019 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alisema asilimia 81.5 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo wamefaulu huku ufaulu wa masomo yote ukiwa juu ya wastani.

Mara imeungana na mikoa mingine 10 iliyofanya vibaya kitaifa ya Manyara, Tabora, Dodoma, na Singida. Mikoa mingine iliyoingia katika orodha hiyo ya aibu ni Songwe, Kigoma, Tanga, Lindi, na Shinyanga.

Kati ya mikoa 10 ya mwisho iliyoingia katika orodha ya mwaka huu, mikoa nane imeendelea kubaki katika nafasi hizo huku miwili ya Singida na Sinyanga ikiwa ni mipya.

 

 

Mfanano wa matokeo ya 2018 na 2019

Wakati Mara ikijikongoja mkiani, baadhi ya halmashauri zake vimefanya vibaya pia na kuchangia mkoa huo kufanya vibaya kitaifa licha ya juhudi mbalimbali zinazofanyika na Serikali kutoa elimu bila malipo. 

Mathalani, mpangilio wa Halmashauri kwa ubora wa ufaulu katika mtihani wa PSLE 2019 unaonyesha Mara imeingiza Wilaya mbili Butiama ambayo imeshika nafasi ya 181 na Rorya (184) zikiwa juu kidogo ya Halmashauri ya Morogoro Vijijini ambayo imeshika mkia kitaifa kati ya halmashauri 186 Tanzania bara.

Hata mwaka jana, mkoa huo uliingiza halmashauri mbili za Butiama na Musoma Vijijini katika orodha hiyo ya aibu.

Anguko la Mara katika matokeo hayo halikuishia ngazi ya mkoa na halmashauri limeshuka hadi katika ngazi ya chini ya shule ambapo imeingiza shule moja ya Bubombi miongoni mwa shule 10 zilizofanya vibaya kitaifa.

Bubombi ipo katika Wilaya ya Rorya ambapo kiwilaya, kimkoa na hata kitaifa haijafanya vizuri, ikiwakilisha shule zingine zilizofanya vibaya katika mkoa huo licha ya shule hizo kutokuwepo katika kundi la 10 za mwisho kitaifa.

Mwaka jana pia mkoa huo uliingiza shule moja ya Magana iliyopo katika Wilaya ya Butiama katika kundi hilo, ambapo mwaka huu haijajirudia tena.


Zinazohusiana:


Wakati viongozi wa Mara wakitafakari namna ya kujinusuru na matokeo mabovu katika mtihani wa 2019, huenda wakapata ahueni kidogo kwa sababu mkoa huo umefanya maajabu yake ambayo yameacha alama na kuwasaulisha watu kama mkoa huo umeshika nafasi ya mwisho kitaifa.

Mara imefanikiwa kutoa wanafunzi watano kati ya 10 bora kitaifa ambao wote wametoka Shule ya Msingi ya Graiyaki, wakiongozwa na mtahiniwa wa shule hiyo, Grace Manga ambaye ameongoza kitaifa.

Pia mkoa huo uliokuwa na shule 815 zilizofanya mtihani, imetoa shule mbili za Graiyaki na Twibhoki ambazo zimeingia 10 bora huku shule ya Graiyaki ikishika nafasi ya kwanza kitaifa.

Dk Msonde alizitaja shule nyingine tisa zilizofanya vizuri kuwa ni Kemebos ya Kagera, Little Treasures (Shinyanga) na Musabe (Mwanza). Nyingine ni Tulele ya mkoani Mwanza, Kwema Modern (Shinyanga), Peaceland (Mwanza), Mugini (Mwanza) na Rocken Hill ya Shinyanga. 

Imeshika nafasi ya mwisho kitaifa katika mtihani wa darasa la saba kama ilivyokuwa mwaka jana. Picha|DW.

Nini kimeifikisha Mara hapo ilipo

Ufaulu wa Mara hautofautiani sana na mikoa mingine ya kanda ya ziwa, kwani mikoa hiyo inabebwa zaidi na shule binafsi ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika matokeo ya kitaifa.

Mathalani, mwaka huu shule zote zilizoingia 10 bora zimetoka kanda ya ziwa licha ya kuwa kanda hiyo imeingiza mikoa miwili ya Kagera na Simiyu katika mikoa 10 iliyofanya vizuri huku ikiingiza mikoa miwili ya Shinyanga na Mara kwenye orodha ya mikoa iliyofanya vibaya. 

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya elimu wameiambia Nukta kuwa watoto wanaoishi kanda ya ziwa wanakabiliwa na changamoto ya kukatisha masomo na kujiingiza katika shughuli za uchimbaji madini, uvuvi na kuchunga mifugo na wengine kuolewa katika umri mdogo jambo linalowafanya washindwe kuhudhuria masomo darasani.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Utafiti wa Kujipima kwa njia ya kujifunza Afrika unaoratibiwa na Chuo Kikuu cha Aga Khan kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Oxford cha nchini Uingereza umebaini kuwa kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi katika shule za msingi kunasababisha na kutokuwepo kwa mahusiano mazuri kati ya walimu na wanafunzi.

Juhudi za kumpata Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima kuelezea hali hiyo na jinsi walivyojipanga kutoka katika mkwamo huo hazikufanikiwa kwa sababu simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa.