October 6, 2024

Marekani yaanza kuchukua taarifa za mitandao ya kijamii waombaji wa viza

Utaratibu huo utahusu waombaji wote wa viza wanaotaka kuhamia nchini humo na wanaotaka kuzuru kwa muda mfupi

  • Mpango huo mpya unahitaji muombaji kuwasilisha taarifa za Facebook, Twitter and Youtube kwa miaka mitano iliyopita.
  • CNN imeripoti kuwa utaratibu huo mpya umeshaanza kufanya kazi. 

Iwapo una mpango wa kwenda Marekani siku za hivi karibuni basi jiandae mapema kutoa taarifa zaidi ya zile ulizotarajia baada ya Serikali ya Marekani kuanza kuomba taarifa za akaunti za mitandao ya kijamii kwa takriban waombaji wote wa viza za kuingia nchini humo.

Mapema mwishoni mwa wiki iliyopita Marekani ilitangaza kuwa itaanza kuomba taarifa za miaka mitano za waombaji wa vibali hivyo vya kuingia au kuishi katika taifa hilo tajiri duniani. 

Shirika la habari la Marekani la CNN limeeleza kuwa taarifa iliyotolewa na serikali ya nchi hiyo inabainisha kuwa tayari imeshaanza kuomba taarifa hizo mbali na zile zilizokuwa zikihitajika hapo awali kama taarifa binafsi, historia ya safari za nyuma, na anuani ambazo ulishawaji kuzitumia. 

“Taarifa hizi zitasaidia jitihada za kuwatambua vema waombaji wa viza hizo na kuthibitisha kuwa wanaoomba ndiyo wenyewe,” imenukuliwa taarifa hiyo na CNN.


Soma zaidi: Haviruhusiwi: Ubalozi wa Marekani Tanzania wapiga marufuku vifaa vya kielektroniki, mikoba mikubwa


Shirika hilo linakadiria kuwa zaidi watu milioni 15 wataathirika na mpango huo mpya wa Marekani ambayo Rais wake Donald Trump amepania kuweka vigezo vikali ili kudhibiti wahamiaji katika taarifa hilo la magharibi. 

Mpango huo wa kuchukua taarifa za mitandao ya kijamii za waombaji wa viza ulitolewa Machi mwaka jana lakini haukuanza kutekelezwa mapema.

Baadhi ya wanaharakati nchini humo wanasema hatua hiyo imelenga kuminya haki za watu wanaotaka kuingia nchini humo na huenda isizae matunda katika kudhibiti wahamiaji kama inavyotarajiwa.

Katika utaratibu mpya, watumiaji wanaotaka kuhamia na wanaotaka kuzuru tu wataombwa taarifa za miaka mitano za Facebook, Twitter, Youtube na “kujitolea” taarifa za mitandao mingine ambayo haijaorodheshwa ndani ya fomu hizo mpya, Shirika la habari la CBS News imebainisha. 

Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa na msimamo mkali katika udhibiti wa wahamiaji nchini humo ukiwa mpango wa kujenga ukuta mpakani na Mexico unaopingwa vikali na Chama cha Democrat. Picha|NDTV.com.