October 6, 2024

Marekani yaipongeza Nukta Africa mapambano ya habari za uzushi

Imeipongeza kwa mchango wake wa kukabiliana na habari za uzushi kwa kutoa mafunzo ya uthibitishaji habari na ujuzi wa kidijitali kwa waandishi wa habari na vijana wa Tanzania.

  • Yasema kampuni hiyo inafanya kazi nzuri ya kuongeza ujuzi kwenye jamii kuhusu habari za uzushi na matumizi ya dijitali
  • Imesema ujuzi huo wa uthibitishaji habari na kidijitali ni muhimu kwa ukuaji wa vyombo vya habari.
  • Nukta Africa yasema itandelea kufanya kazi wa bidii na weledi kuifikia jamii kupitia tasnia ya habari.

Dar es Salaam. Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umeipongeza kampuni ya Nukta Africa kwa mchango wake wa kukabiliana na habari za uzushi kwa kutoa mafunzo ya uthibitishaji habari na ujuzi wa kidijitali kwa waandishi wa habari na vijana wa Tanzania. 

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani alioutoa leo Mei 3, 2021 amesema katika kukabiliana na ongezeko la usambaaji wa taarifa zisizo sahihi na za uzushi kupitia mitandao ya kijamii, amefurahishwa na jitihada zinazofanywa kukabiliana na changamoto hiyo nchini.  

“Ninapongeza kazi inayofanywa na taasisi kama Nukta Africa, ambayo kwa msaada wa Serikali ya Marekani, inakabiliana na uenezaji wa taarifa za uongo kwa kuwapatia waandishi wa habari na vijana ujuzi wa kuthibitisha ukweli wa taarifa (fact-checking) na ujuzi wa kidijitali (digital literacy skills),” amesema Wright.

Nukta Africa ambayo inamiliki tovuti ya habari ya nukta.co.tz na maabara (Nukta Lab) hufanya mafunzo kwa wanahabari na wadau wengine katika uandishi wa habari za takwimu, uthibitishaji habari na matumizi ya dijitali katika kuzalisha habari zenye mchango mkubwa kwa jamii. 

Miaka ya hivi karibuni imekuwa ikifanya kazi na washirika kama Internews Tanzania katika mradi wa Boresha Habari unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID). 

Balozi huyo amesema ametiwa moyo na vyombo kadhaa vipya vya habari vya Tanzania ikiwemo Nukta Africa vilivyokubali kupokea teknolojia mpya katika uendeshaji na ufanyaji wake biashara. 


Soma zaidi: 


Amesema Serikali ya Marekani inafadhili programu kadhaa za kusaidia maendeleo ya vyombo vya habari, zinazofanya kazi na wamiliki wa vyombo vya habari katika kubuni na kuboresha mbinu mpya za kibiashara zenye ufanisi zaidi. 

“Nina matumaini makubwa kwamba jitihada hizi zitazaa matunda,” amesema Wright. 

Amesema amefarijika na hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan za kuondoa baadhi ya vikwazo kandamizi kwa vyombo vya habari na taarifa za uwepo wa mchakato wa kuunda kamati ya kupitia sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na zile zinazokwaza uhuru wa habari na vyombo vya habari.

Mkuu wa Utawala na Fedha wa Nukta Africa, Maphosa Banduka amesema kampuni hiyo imefarijika kuona wadau kama Marekani kutambua kazi wanazofanya hasa katika kupambana na habari za uzushi kwenye jamii na kuongeza uelewa wa masuala ya matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kupashana habari.

“Hii imetupa nguvu zaidi ya kuendelea kufanya kazi zetu kwa weledi na kasi ili tuzidi kuwa sehemu ya kutoa mchango wetu katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla kupitia tasnia ya habari,” amesema Banduka. 

Amesema wataendelea kushirikiana na wadau wote nchini kuhakikisha tasnia ya habari nchini inaheshimika na inatimiza wajibu wake kwa kuzingatia taaluma na uhuru wa vyombo vya habari.