September 29, 2024

Marekani yarejea rasmi katika mkataba wa Paris

Ni baada ya kujiondoa mwaka jana chini ya utawala wa Rais mstaafu Donald Trump.

  • Ni baada ya kujiondoa mwaka jana chini ya utawala wa Rais mstaafu Donald Trump.
  • Mkataba huo ulisainiwa 2015 ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Marekani imethibitisha rasmi kurudi katika makubaliano ya mkataba wa Paris, jambo linalodhihirisha mwanzo mpya katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi duniani.

Uamuzi huo umefanyika kwenye hafla iliyofanyika Februari 19, 2021 katika ofisi za Umoja wa Mataifa (UN), Marekani, baada ya Rais Joe Biden wa Marekani kuchukua wadhifa mnamo Januari 20, na kuanzisha mchakato wa siku 30 wa kurejea katika makubaliano hayo.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Mjumbe Maalum wa Rais Biden kuhusu tabianchi, John Kerry, kwa njia ya mtandao, Marekani imeendelea kuonyesha utayari wa kuungana tena na ulimwengu katika kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi wakati huu na hata kwa vizazi vijavyo.

Kujiondoa kwa Marekani katika mkataba huo, ambako kulifanyika rasmi Novemba mwaka jana, kuliifanya nchi hiyo kuwa ya kwanza na ya pekee kujiondoa katika makubaliano ya ulimwengu yaliyopitishwa mwaka 2015 nchini Ufaransa.


Soma zaidi: 


Katibu Mkuu wa UN, Antonio Geterres amesema kurejea kwa Marekani katika mkataba wa Paris kunaashiria “siku ya matumaini”.

Akizungumza katika hafla hiyo, Guterres amesisitiza kuwa kitendo hicho ni “habari njema” kwa Marekani na ulimwengu.

Guterres pia amemkumbusha Kerry, tukio la mwaka 2016 ambapo mjumbe huyo maalum wa Rais wa Marekani, alisaini mkataba wa huo wa Paris akiwa na mjukuu wake ili kuonesha kuwa, huo haukuwa tu mkataba wa kizazi hiki, bali pia kizazi kijacho.

Mkataba huo wa umeweka makubaliano ya kimataifa yanayolenga kupambana na utoaji wa gesi zinazochafua mazingira has a zinazotoka viwandani pamoja na athari nyinginezo za mabadiliko ya tabia nchi.